Thursday, 26 May 2016
BODI TUME YA VYUO VIKUU YATUMBULIWA
SERIKALI imevunja Bodi ya Wakurugenzi wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na kuwasimamisha kazi watendaji wakuu kwa kudahili wanafunzi wa kidato cha nne kwenda kusomea shahada ya sayansi katika chuo kikuu.
Hadi jana, wanafunzi waliobainika kutokuwa na sifa hata ya kusomea cheti cha ualimu, lakini wanasoma shahada ya elimu ya sayansi, walifikia 489 katika Chuo Kikuu cha St. Joseph cha Songea.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alitangaza uamuzi huo jana mjini hapa, alipokutana na waandishi wa habari.
Alisema waliosimamishwa kazi ni Profesa Yunus Mgaya ambaye ni Mtendaji Mkuu wa TCU na Dk. Savinus Maronga, ambaye ni Msimamizi wa Ubora na Ithibati Vyuo Vikuu.
Wengine ni Rose Kiishweko ambaye ni mdahili wa wanafunzi na Kimboka Instanbul ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi Usajili.
Alisema serikali imeamua kuivunja bodi hiyo baada ya kubaini kuwa wanafunzi waliodahiliwa katika chuo hicho ni wenye daraja la nne pointi 32.
Hivi kweli wanafunzi kama hawa unawadahili na kuruhusu wasomee sayansi, tutakuwa na wanasayansi wa aina gani? alihoji.
Waziri huyo alisema cha kusikitisha zaidi wanafunzi hao walikuwa wakipewa mikopo ya elimu juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu.
Alisema hayo yalibainika baada ya kufanyika uchunguzi kutokana na awali wanafunzi hao kuhamishwa katika vyuo vingine ili waendelee na masomo yao, baada ya chuo chao kufungwa kutokana na kutokuwa na sifa ya kutoa masomo hayo.
Alisema baada ya wanafunzi hao kuhamishwa katika vyuo mbalimbali, walibainika hawana uwezo wa kile wanachosoma, hivyo kurudishwa nyuma kwa mwaka mmoja au zaidi.
Profesa Ndalichako alisema wanafunzi waliohamishiwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa mwaka wa tatu walionekana hawana uwezo na hivyo kurudishwa mwaka wa pili kutokana na uwezo wao kuwa chini ukilinganisha na wale wa UDOM.
Alisema waliohamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine wa mwaka wanne nao walirudishwa nyuma mwaka wa tatu kutokana na sababu hiyo hiyo na wengine kulazimika kupewa masomo ya muda wa ziada.
‘’Sasa inafikia mwanafunzi wa elimu ya juu anapewa masomo ya ziada ili aweze kuendana na wenzake je huyo ana sifa ya kuwa nafasi hiyo?’’ alihoji.
Waziri huyo alisema hali hiyo iliwashitua, hivyo wakaamua kufanya ufuatiliaji zaidi katika sehemu mbalimbali juu ya viwango vya elimu vya wanafunzi hao.
Alifafanua kuwa walipokwenda kufuatilia Baraza la Mitihani la Taifa ,ilibainika kuwa wanafunzi hao wengi wao hawana sifa hata ya kusomea cheti cha ualimu.
“Tena wengine wamesoma masomo ya biashara, lakini wamedahiliwa kusomea sayansi tunaenda wapi,’’ alisema.
Alisema baada ya kulitambua hilo waliamua kupeleka taarifa TCU kuchukua hatua, lakini Mwenyekiti wa Bodi hiyo alikataa.
‘’Baada ya kutoa taarifa kwa rais amekubali kuivunja bodi hiyo na kwa sasa wameshateuliwa wengine kushika nafasi hiyo katika kipindi cha mpito,’’ alisema.
Alisema walioteuliwa kujaza nafasi hizo ni Profesa Eleuther Mwageni, ambaye atakaimu nafasi ya Katibu Mkuu Mtendaji (TCU),
Awali, Eleuther alikuwa Naibu Makamu Mkuu wa Utawala na Fedha wa Chuo Kikuu cha Ardhi.
Dk. Kokubelwa Katunzi Mollel, ameteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi wa udahili na nyaraka. Kabla ya hapo alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Hata hivyo, waziri huyo alisema tayari uchunguzi umeshaanza kwa kushirikiana na TAKUKURU kupitia vyuo vyote vikuu, ili kubaini wanafunzi ambao hawana sifa na wanasoma.
Alisema pamoja na hilo wapo wanafunzi ambao wanapata mikopo wa elimu ya juu, lakini hawastahili hao nao dawa yao ipo njiani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment