Thursday, 26 May 2016

MJADALA MKALI WAIBUKA SAKATA LA WAKULIMA NA WAFUGAJI


MVUTANO mkali baina ya wabunge wanaotoka kwenye maeneo ya wafugaji na wakulima umelitikisa bunge na kusababisha mgawanyiko baina ya wabunge wanaotoka kwenye maeneo hayo.

Hali hiyo iliibuka wakati wa majadiliano kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo wabunge wanaotoka maeneo ya wakulima waliitaka wizara hiyo kudhibiti mifugo inayoingia mashambani na kwenye mapori ya akiba.

Pia, wabunge hao waliitaka serikali kuongeza nguvu za kukabiliana na majangili kwa kuweka sheria kali, ikiwemo kupigwa risasi pindi majangili hao wanapokamatwa kwenye maeneo ya hifadhi.

Aidha, walisisitiza kuwa lazima kuwepo na udhibiti wa mifugo inayoingia kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori na kuhakikiwa kwa mipaka inayotenganisha vijiji na hifadhi hizo.

Akichangia makadirio hayo, mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy, alisema hakuna sababu kwa serikali kuwaacha wafugaji kuchunga mifugo kiholela na lazima wawekewe utaratibu maalum.

Alisema wafugaji wamekuwa wakivamia mapori ya akiba na hifadhi mkoani Katavi, hivyo aliiomba wizara kufanya doria kwenye maeneo hayo kuwadhibiti wafugaji na kuacha kuwabembeleza.

Aliongeza kuwa kutokana na kutokuwepo kwa mfumo thabiti wa kudhibiti mifugo, lazima serikali iandae utaratibu maalum wa kutoza kodi ya mifugo kwa wafugaji.

“Hakuna muda wa kubembelezana hapa, lazima wafugaji wadhibitiwe, ikiwemo kutozwa kodi ya mifugo yao,” alisisitiza.

Mbunge huyo alisema katika kukabiliana na vitendo vya ujangili, lazima serikali itoe adhabu kali kwa majangili pindi wanapokutwa kwenye hifadhi, ikiwemo kupigwa risasi.

“Unamkamata mtu na kidhibiti, halafu unampeleka polisi ili iweje? kama kuna kidhibiti hakuna muda wa kupoteza, majangili hawa wakikutwa kwenye hifadhi wapigwe risasi,” alisema.

Kessy aliiomba serikali kutoyachoma moto meno ya tembo yaliyokamtwa na kuhifadhiwa kama ilivyofanya nchi ya Kenya.

Alisema meno hayo ni vyema yakauzwa kisha fedha zitakazopatikana zitumike kununulia vitendea kazi vya kupambana na ujangili.

Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini - CHADEMA)  alisema lazima maeneo yaliyohifadhiwa yatumike kwa shughuli za kiuhifadhi na si wafugaji kuachiwa wakiyavamia.

Aliiomba serikali kuweka utaratibu maalum ili kuwawezesha wafugaji kuendesha shughuli zao kwa kutoingilia maeneo yaliyohifadhiwa.

Kwa upande wake, James Ole Millya (Simanjiro - CHADEMA), alidai serikali imekuwa ikiwaonea wafugaji kwa kuwahamisha kila kukicha pasipo kuwatengea maeneo maalum.

Alisema serikali imekuwa ikiwanyanyasa wafugaji kwa kukamata mifugo yao kisha kutozwa kiwango kikubwa cha faini.

“Lazima tusema ukweli, wafugaji tumekuwa tukinyanyasika kwa kuhamishwa kwenye maeneo mbalimbali, huku mifugo yetu ikikamtwa, hali hii inasikitisha,” alisema Millya.

Dk. Ester Kikwembe (Kavuu - CCM), aliiomba serikali kufanya juhudi za haraka kuumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji ulioko kwenye kata ya Ikuba.

Alisema mgogoro huo ulijitokeza baada ya wafugaji kuhamishwa bila kuonyeshwa maeneo wanayopaswa kwenda, hivyo kusababisha mifugo kuingia katika mashambani.

Alikadhalika, Profesa Norman Sigalla (Makete -CCM) alisema lazima wafugaji waondokane na dhana ya uchungaji mifugo.

MBUNGE ATAKA UZAZI WA MPANGO KWA TEMBO

Marwa Getere (CCM), alishangazwa na namna ambavyo tembo wanavyovamia mashamba kisha kuharibu mazao ya wakulima, hivyo alihoji kwa nini wanyama hao wasiwekewe utaratibu wa uzazi wa mpango.

“Hivi hao tembo hawana utaratibu wa uzazi wa mpango? Wamekuwa wakivamia mashamba na kusababisha hasara kwa wakulima, hivyo serikali lazima iongeze juhudi za kukabiliana na tatizo hilo,” alisisitiza Getere.

Alisema tembo wamekuwa wakivamia mashamba, lakini wizara  haijalipa fidia zaidi ya sh. milioni 400 kwa wakazi wa jimbo lake, ikiwa ni malipo ya kufidia hasara iliyosababishwa na wanyama hao.

No comments:

Post a Comment