Thursday, 26 May 2016

YONO YAKUSANYA BILIONI TATU ZA WALIOKWEPA KODI


KAMPUNI ya udalali ya Yona Auction Mart, iliyopewa  dhamana ya kukusanya kodi na serikali,  imetoa ripoti  ya maendeleo ya sakata la  makontena 329  ya wafanyabishara waliokwepa kulipa kodi katika Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari jana, hadi sasa kampuni hiyo imeshakusanywa zaidi ya sh. bilioni tatu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Yono Auction Mart, Stanley Kevela, alisema thamani ya makontena hayo ilikuwa sh. bilioni 18, ambazo wafanyabishara hao walitakiwa kulipia kodi.

Alisema wafanyabishara waliokuwa wanadaiwa kodi ni 24, ambapo kati yao, saba wamelipa na 11 bado hawajalipa huku wengine wakiwa wametoroka pamoja na mali.

Aliwataja wafanyabishara, ambao mpaka sasa wamelipa kodi na faini kuwa ni  Zulea Ally,  aliyekuwa akidaiwa sh. milioni  16.8, Omary Hussein  sh. milioni  29.4, Libas Fashion sh.milioni 26.6, Farid Abdalah sh.milioni 52.2, Ally Awes  sh. milioni 55.5, Zulea Ally sh. milioni  75.5 na Issa  Alli Salum sh. milioni 94.5.

“Kampuni zingine ambazo zilikuwa na madeni makubwa ni TAFFA, ambayo ilitupeleka mahakamani, hivyo kesi bado inaendelea. Kampuni hii inadaiwa sh. bilioni 7.4, lakini kwa kuwa bado kesi iko mahakamani, hatujagusa mali zake, lakini kama tutashinda kesi, basi tutauza mali zake zote ili kulipa,”alisema Kevela.

Pia, alisema kampuni ya  kichina ya TIFFO, iliyokuwa ikidaiwa sh.bilioni  1.5,  imemaliza kulipa deni  lake, baada ya mali zake kupigwa mnada huku kampuni ya Rotary, pia mali zake zinaendelea kuuzwa ili kufidia deni la sh. bilioni   7.8.

“Fedha ambazo tumekusanya mpaka sasa ni sh. bilioni tatu na tunashikilia mali zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 10, ili kufidia deni lote.  Tunaamini kwamba hadi kufikia mwezi ujao tutakuwa tumekusanya fedha zote za makontena 329,”alisema Kevela.

Katika hatua nyingine, Kevela  alisema tayari Kampuni ya Yono imeliandikia barua Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ili kuendesha msako mkali kwa wafanyabishara saba waliotoroka na mali zao katika Bandari ya Nchi Kavu  (ICD) ya Azam.

“Tumemuandikia barua Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ili tuweze kushirikiana pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuendesha msako mkali wa wafanyabishara hao waliotoroka.  Tunaomba wananchi kutusaidia kufichua mali zao ,”alisema  Kevela.

Kevela pia alitoa wito kwa taasisi za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya ujenzi, kujitokeza kununua mali, hususan mabati yanayoshikiliwa, ambayo yanauzwa kwa mnada na kwamba kampuni hizo  zitauziwa kwa kiwango nafuu.

Sakata la makontena 329, lililiibuliwa na Rais Dk. John Magufuli,  baada ya kubaini uozo mkubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo ilibainika yalipitishwa bila kulipiwa kodi.

No comments:

Post a Comment