KAMPUNI ya
Reli Tanzania (TRL), imewaonya wananchi, hususan wenye tabia ya kudandia treni
baada ya milango kufungwa.
Imesema mtu
yeyote atakayetiwa hatiani kwa kosa hilo, adhabu yake ni kifungo cha miezi sita
jela.
TRL imesema tayari
jeshi la polisi limeanza operesheni ya kuwasaka abiria wasiotaka kufuata sheria
za kuingia kwenye usafiri huo, badala yake wamekuwa wakidandia mabehewa baada ya milango kufungwa.
Aidha, kampuni
hiyo imetangaza neema kwa wasafiri wa
treni ya Dar es Salaam, kuwa imepanga kununua treni mpya ndani ya mwaka ujao wa
fedha, ambayo itatoa huduma hiyo kwenye maeneo mbalimbali.
Akizungumza
jana, Dar es Salaam, Meneja Usafirishaji Abiria wa TRL, Iddi Mzungu, alisema katika
siku za hivi karibuni, kumeibuka tabia ya baadhi ya abiria kudandia kwenye mabehewa
baada ya milango ya treni kufungwa na kusisitiza kuwa, atakayebainika
atapelekwa mahakamani na kufungwa miezi sita jela.
''Tunaomba
abiria wafuate sheria za matumizi ya treni. Agosti 3, mwaka jana, aina hii ya uvunjaji wa sheria ilisababisha
mtu mmoja kupoteza maisha baada ya kuning’inia na kugongwa na geti la kuingilia
stesheni,''alisema.
Wakati huo
huo, Mzungu amesema tayari mamlaka hiyo imekwishaandaa mpango wa kuletwa treni
nyingine mpya, ambayo itasaidia kupunguza adha ya usafiri katika jiji la Dar es
salaam.
Alisema treni
hiyo ya kisasa itakuwa na uwezo wa kutumia mafuta kidogo pamoja na kuwa na uwezo
wa kutembea haraka zaidi.
“Tulishaandaa
mpango, tunaagiza treni mpya, ambayo
itaondoa changamoto ya usafiri Dar es
salaam, itakuwa ya kasi na isiyo na matumizi makubwa ya mafuta,” alisema.
Akielezea
mkakati wa jeshi la polisi reli juu ya
kudhibiti matukio hayo, mwakilishi wa jeshi hilo, Kamanda Frank Gadau,
alisema tayari operesheni imekwishaanza, ambapo abiria atakayebainika kukiuka sheria ya usafiri huo, atakamatwa na kufikishwa
mbele ya sheria .
No comments:
Post a Comment