Wednesday 8 June 2016

JELA MIEZI SITA KWA KUTUMIA BARABARA ZA DART

JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, limesema limewafikisha mahakamani madereva wawili wa pikipiki kwa kosa la kupita katika njia ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART) na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita kila mmoja.

Madereva hao ni Hassan Mohamed, mkazi wa Tegeta na Rashid Sheha, mkazi wa Kimara. Madereva wengine kesi zao zinaendelea kusikilizwa.

Mohamed (30), alikuwa akiendesha pikipiki yenye namba za usajili MC 299 ABS, aina ya Sunlag wakati Sheha (45), alikuwa akiendesha pikipiki namba MC 379 ASV, aina ya boxer.

Akizungumza jana, Dar es Saalam, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alisema hatua hizo zitasaidia kupunguza makosa ya matumizi ya barabara hizo.

Kamanda Mpinga alisema hatua hiyo itakuwa ikichukuliwa na hakutakuwa na masuala ya kulipa faini kwa kosa la matumizi ya barabara hizo.

"Kinachofanywa kwa sasa ni kwamba, dereva atakayekosea atapigwa picha katika ubao wetu kuonyesha kosa alilofanya na itasaidia kuwa katika kumbukumbu ya polisi,"alisema.

Alisema madereva watakaokamatwa wataswekwa mahabusu kwa ajili ya kufikishwa mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine.

Aidha, aliongeza kuwa jeshi la polisi halijawaelekeza askari wa  usalama barabarani kukamata kiwango cha makosa kumi kila siku.

Alisema hakuna jambo kama hilo na kwamba, ni taarifa hizo ni za uongo na kwamba, kuna makosa mengi yanatokea hivyo hakuna kiwango cha askari kukamata makosa hayo.

"Kuna makosa kama vile ya kutanua, wanavuka wakati taa nyekundu imewaka, madereva hawavai kofia, kuna wengine hawana leseni, sasa utasemaje idadi ya makosa," alihoji.

No comments:

Post a Comment