Sunday, 5 June 2016

POLISI DAR WAANZA MSAKO WA MADEREVA WALEVI


JESHI la Polisi mkoa wa Ilala, jijini Dar es Salaam, limetangaza kuanza kwa msako mkali wa madereva walevi ili  kupunguza ajali zinazochangiwa na uzembe.

Pia, jeshi hilo limesema litawakamata abiria wanaopanda pikipiki bila kuvaa kofia ngumu na kuwachukulia hatua, sambamba na waendeshaji wake.

Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya, alisema jana kuwa, wamejipanga vya kutosha kuendesha operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na kusambaza vifaa maalumu vya kuwabaini madereva walevi.

Alisema operesheni hiyo itakuwa ya kushtukiza kwa madereva barabarani, ambapo ripoti zao zitakuwa zikihifadhiwa na iwapo itabainika kwamba wamekubuhu, watawachukulia hatua kali za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya leseni.

“Ninawaonya madereva walevi waache mara moja.Operesheni hii ni kubwa na tunavyo vifaa vya kutosha vya kupimia ulevi, ambavyo  tutawapa polisi  wa Kikosi cha Usalama Barabarani. Wale ambao wanalala na pombe kichwani basi wasiendeshe gari kabisa siku hiyo,”alisema.

Akizungumzia kuhusu abiria wasiovaa kofia ngumu, alisema utaratibu umebadilika,hivyo hawatasita kumkamata abiria, ambaye atakuwa anakiuka utaratibu huo.

“Awali tulikuwa tunamkamata dereva wa bodaboda tu,lakini hivi sasa hata abiria, ambaye hajavaa kofia ngumu atakamatwa. Hivyo nawaonya wananchi wanaotumia pikipiki, kudai kofia ngumu kabla ya kukodi, la sivyo wataingia matatizoni,”alisema.

Akitoa ripoti za ajali barabarani zilizotokea katika wilaya ya Ilala, katika kipindi cha Januari na Mei, mwaka huu, Nkondya alisema watu 40 walikufa katika matukio tofauti.

Alisema vifo hivyo vilitokana na ajali 845, zilitotokea ambapo kati ya waliokufa, 37 ni wanamume na watatu ni wanawake huku majeruhi wakiwa ni 463.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, kati ya majeruhi hao, wanawake ni 132 na wanaume ni 522.

“Ripoti inaonyesha kuwa, magari binafsi yaliyohusika katika ajari hizo ni 630, mabasi makubwa mawili, daladala 208,  malori, magari ya kuzoa taka na mchanga  87, pick up 53 na pikipiki  310,”alisema.

Mkondya alisema chanzo cha ajali hizo kwa asilimia 90, zinatokana na uzembe wa binadamu, hasa madereva.

Kamanda Mkondya alitoa wiki tatu kwa wamiliki wa magari  mabovu, hasa ya kubeba taka, malori na mengine, kuyatengeneza  haraka   kwani baada ya muda huo kumalizika yatakamatwa na kufungiwa.

“Natoa wito kwa madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani kwani msako mkali umeanza na wazembe hawatasalimika,”alionya.

No comments:

Post a Comment