Monday, 6 June 2016
UFAGIO WA CHUMA WAPITA UHAMIAJI, MAOFISA 59 WAHAMISHWA
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imewahamisha maofisa na askari wa Idara ya Uhamiaji 59, kutoka ofisi ya mkoa wa Dar es Salaam na wilaya zake na kupelekwa sehemu mbalimbali nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, alisema uhamisho huo umefanyika ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Idara ya Uhamiaji.
Meja Jenerali Rwegasira alisema kazi ya kuwahamisha maofisa wa Idara ya Uhamiaji inaendelea kufanyika nchi nzima, ikiwa ni hatua za kuboresha utendaji kazi, hivyo kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
"Watumishi wote waliopewa uhamisho wanatakiwa kuripoti kwenye vituo vyao vipya mara moja na mtumishi yeyote atakayeshindwa kuripoti kwa visingizio mbalimbali, atachukuliwa hatua kali za kinidhamu, ikiwemo kuachishwa kazi," alisema Rwegasira.
Alipoulizwa kuhusiana na uhamisho huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuph Masauni, alisema kazi ya kusafisha Idara ya Uhamiaji ni endelevu na kwamba bado inaendelea.
"Kazi hiyo ni endelevu na bado tunaendelea kuchukua hatua dhidi ya watumishi hao, lengo likiwa kuleta ufanisi katika utendaji kazi," alisema Masauni alipozungumza na gazeti hili.
Wiki iliyopita, Masauni aliagiza kupewa barua za kuondolewa kazini mara moja, watumishi wa Idara ya Uhamiaji, kitengo cha upelelezi, ambao wameshindwa kwenda sambamba na kasi iliyopo.
Mhandisi Masauni alitoa kauli hiyo mjini Dodoma, baada ya kumaliza kikao na wawakilishi wakuu na wasaidizi wa vyombo vyote ndani ya wizara hiyo, ambao ni Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji.
Alisema ndani ya Idara ya Uhamiaji, kumekuwepo na watumishi ambao wanachafua taswira na kazi nzuri inayofanywa na jeshi hilo hapa nchini na kwamba, watendaji hao ni kutoka kitengo cha upelelezi, ambao wamekuwa wakishindwa kusimamia vizuri udhibiti wa mipenyo ya mipakani, hivyo kuachia wahamiaji haramu wakiingia kupitia mipaka hiyo.
Pia, alisema wamegundua kuna mapungufu kwa maofisa uhamiaji katika kitengo cha uchunguzi, ambao wana jukumu la kwenda kwenye baadhi ya kampuni na mashirika kufanya msako wa wahamiaji haramu wanaoharibu kazi nzuri ya jeshi hilo ya kushughulika na wahamiaji haramu.
“Kama tunaona kuna watu ambao hawaendi sambamba na kasi tunayoitaka, ikiwemo wengi waliopo jiji la Dar es Salaam, tumeagiza waondoshwe mara moja, kwa hiyo tutaangalia wale ambao tutajiridhisha kwamba hawaendi na kasi yetu, waondoke wakatafutiwe sehemu, ambayo wanaweza kufanya kazi, hii ndio awamu tano,” alisema Masauni.
Katika hatua nyingine, serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba wa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi askari eneo la Kunduchi, Mikocheni na Kituo cha Polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam, unaohusisha majengo mbalimbali ya mwekezaji ambayo jeshi limeingia naye mkataba.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Rwegasira, alisema mradi huo ni mkubwa na wa muda mrefu, hivyo ameliagiza jeshi hilo kuuwasilisha mkataba huo ambao utekelezaji wake unaendelea ili aweze kuufahamu vizuri.
Mkataba huo unalihusisha Jeshi la Polisi na Mwekezaji wa Kampuni ya Mara World Tanzania limited.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment