Monday, 6 June 2016

SENDEKA: MSICHAGUE WABUNGE ILI WAKASUSIE VIKAO NA KUSHINDA BAA


WATANZANIA nchini kote, wameaswa kutotumia hasira katika kuchagua wawakilishi wao kwa nafasi muhimu na nyeti za urais, ubunge na udiwani ili kuepuka hatari ya kujicheleweshea maendeleo yao wenyewe.

Ushauri huo ulitolewa juzi na Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka, wakati akihutubia mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye viwanja vya Mkapa Garden, mjini Kilwa Masoko, mkoani Lindi.

Akitolea mfano, Sendeka alisema hatua ya wabunge wa kambi nzima ya upinzani kususia vikao vyote vya bunge, vinavyoendelea mjini Dodoma, ambavyo vinaongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, inaakisi ukweli kwamba, hawana dhamira njema kwa Watanzania na taifa lao.

“Kwa mfano hapa Kilwa Kusini mlimchagua Bwege (Suleiman Bungara) kuwa mbunge wenu (kupitia chama cha CUF), lakini yeye na wabunge wenzake wa upinzani wamesusia vikao vya bunge,” alisema na kuongeza:

“Kile wanachofanya sasa ni kushinda baa wakiwa wanakunywa bia na kufuatilia vikao vya bunge kwa kuangalia taarifa za habari kama nyinyi. Hivi mbunge wa jinsi hii kwenu ana faida gani?”

Pamoja na kukiri kwamba serikali ya CCM kuna wakati nayo hufanya makosa kama anavyofanya mtu yeyote, lakini hizo ni dosari zinazoweza kurekebishwa na hazipaswi kusababisha kupiga kura za hasira kwa kuwachagua wabunge wa vyama kama CUF, CHADEMA au NCCR – Mageuzi, wasiojua wajibu wao kama Bwege na madhara yake sasa yameanza kuonekana.

Huku akishangiliwa muda wote aliokuwa jukwaani, Sendeka alisema kinachofanywa na wabunge hao ni matokeo ya kupeleka waandamanaji bungeni, badala ya wabunge makini kutoka CCM, ambao wanafahamu wajibu wao wa uwakilishi wa wananchi waliowachagua majimboni au kutoka kwenye makundi ya viti maalumu.

“Mlichokifanya ndugu zangu wa Kilwa Kusini na majimbo mengine walikochagua wapinzani ndiyo hicho, ambacho sasa kinatokea. Wabunge hao pia wanaangalia bunge kupitia kwenye luninga kama nyinyi mliopo hapa. Sasa iko tofauti ipi baina yenu na hao? Nadhani ni vizuri tukajifunza kwamba, tusifanye maamuzi mazito ya kuchagua wabunge kwa hasira”, alisema.

Sendeka aliisifu serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, akisema katika kipindi kifupi, viongozi wake wamethibitisha dhamira yao ya kutaka kuiletea maendeleo Tanzania, kwa kuanza kudhibiti mianya ya rushwa, ufisadi na utumiaji mbaya wa madaraka ya umma.

Sendeka, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), alilitaja jambo jingine lililochukuliwa hatua kwa vitendo na serikali kuwa ni kuzuiwa kwa safari zote za kwenda nje mpaka kwa vibali kutoka Ikulu, hatua inayolenga kuokoa fedha za umma na uamuzi huo unaanzia kwa rais mwenyewe.

Alisema hatua zote zinazochukuliwa na viongozi wa serikali hiyo, zinatokana na uteuzi sahihi wa mgombea urais wa CCM, vinginevyo hali ingekuwa mbaya endapo angeteuliwa Edward Lowassa kugombea nafasi hiyo na kushinda.

Akifafanua kuhusu hilo, Sendeka alisema kukatwa kwa Lowassa katika mbio hizo, kulifanywa kwa makusudi kwa vile Chama kilitanguliza mbele uadilifu ili Tanzania iendelee kuwa kwenye mikono salama, sifa ambayo waziri mkuu huyo wa zamani hana.

Sendeka, aliyeonekana kuteka hisia za mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, alisema pamoja na kufanya kampeni za urais kwa miaka 25, Lowassa alienguliwa katika hatua za kwanza na hatimaye akateuliwa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye hana tuhuma zozote za ufisadi zaidi ya kuwa mwadilifu na mchapakazi hodari.

“Ndiyo maana hata Lowassa mwenyewe alimpigia kura ndani ya kikao cha NEC na pia akampigia kura katika Mkutano Mkuu wa Taifa, lakini siku chache baadaye, alihamia upinzani na akafanikiwa kuwaghilibu akili Watanzania,” alisema.

Sendeka pia alimshangaa Lowassa kwa kujipachika kabila la Kimasai, ingawaje ni Mmeru, akisema  kwamba, aliamua kufanya hivyo akidhani angekubalika kitaifa kwa kutumia kivuli cha Waziri Mkuu aliyekufa kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984, hayati Edward Moringe Sokoine, anayeheshimika nchini kote hadi sasa.

Msemaji huyo wa CCM, aliyekuwa wilayani Kilwa kwa ziara ya siku moja, alirejea jijini Dar es Salaam, jana, huku wilaya zote za mkoa wa Lindi zikimwalika aende akahutubie mikutano zaidi ya hadhara, ambapo ataanzia Ruangwa.

No comments:

Post a Comment