RAIS Dk. John Magufuli ameahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Ubungo Kibangu hadi eneo la River Side, itakakoungana na barabara ya Mandela.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwasaidia waumini wa dini ya kikristo na wakazi wa Ubungo wanaoitumia barabara hiyo kwa ajili ya kuwaunganisha na maeneo mengine.
Dk. Magufuli alitoa ahadi hiyo jana, asubuhi alipotembelea Kanisa la Maombezi, linaloongozwa na Mchungaji Antony Lusekelo (Mzee wa Upako), lililoko Ubungo Kibangu, Dar es Salaam.
Akizungumza katika ibada ya asubuhi ya kanisa hilo, Rais Magufuli alisema barabara hiyo ni kiungo cha waumini wa kanisa hilo, wanaotoka Ubungo na maeneo mengine pamoja na wananchi mbalimbali wanapokuwa kwenye shughuli zao.
Alisema amejionea hali ya barabara baada ya kuitumia kufika kanisani hapo na kwamba, ipo haja ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
Aidha, Rais Magufuli alimpongeza Mzee wa Upako kwa huduma ya maombezi anayoitoa kwa waumini wake na watazamaji wanaofuatilia vipindi vyake vya mahubiri kwa njia ya luninga.
“Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa mahubiri yako, kwa hiyo mahubiri unapoyatoa yanasambaa. Kwa kweli mimi na familia yangu huwa yanatubariki sana, hivyo nataka kukuthibitishia kwamba ninakupenda.
“Ndio maana kuna siku moja ulizungumza kuhusu shida ya barabara yako, ikabidi nitafute mbinu za namna gani tunaweza kuishughulikia kwa utaratibu ulio wazi. Nikamtuma meneja wa barabara wa mkoa wa Dar es Salaam, akaja, akaipitia na akafahamu changamoto zilizopo, akafanya upembuzi yakinifu na usanifu, nataka kukuthibitishia kuwa fedha za kutengenezea barabara hii zipo,”alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati wa waumini.
Kwa upande wake, Mzee wa Upako, alimshukuru Rais Magufuli kwa kulitembelea kanisa hilo na kumuombea heri katika uongozi wake ili aweze kufanikisha azma ya kuliletea taifa maendeleo, ikiwemo kufanikisha mpango wake wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
No comments:
Post a Comment