Tuesday, 30 August 2016

LOWASSA, MBOWE WATIWA MBARONI, WAHOJIWA KWA SAA NNE


POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, inawashikilia viongozi wakuu wa CHADEMA, akiwemo Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowassa, kwa kukiuka agizo la serikali la kutofanya mikutano ya ndani ya kisiasa.
Viongozi hao wakikamatwa jana, katika Hoteli ya Giraffe jijini Dar es Salaam, wakiwa wanapanga mikakati ya maandamano yaliyopigwa marufuku ya Ukuta.
Wengine waliokamatwa ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar, Saidi Issa Mohammed, Katibu Mkuu wa chama hicho, Vincent Mashinji na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika.
Mbali na wabunge na wajumbe wa kamati kuu, wengine waliohudhuria kikao hicho walikuwa ni baadhi ya wenyeviti wa halmashauri na mameya wa majiji na manispaa zinazoongozwa na CHADEMA.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, viongozi na wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA wapatao 178, walikutana kwenye hoteli hiyo kwa ajili ya kupanga mikakati ya chama hicho ikiwemo ya maandamano ya Ukuta.
Alisema polisi walifi ka kwenye hoteli hiyo na kuwakamata viongozi wa chama hicho kwa madai ya kutakiwa kwa ajili ya kuhojiwa.
Alibainisha kuwa viongozi wa chama hicho akiwemo Lowassa walichukuliwa na polisi hadi Kituo Kikuu cha Polisi kuhojiwa. Viongozi hao walifi kishwa kwenye kituo hicho cha polisi saa 9:17 jioni huku
Lissu akiwa na baadhi ya wabunge na wajumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, wakizuiwa kuingia ndani ya kituo hicho.
Katika hali ya kushangaza, baadhi ya wabunge na viongozi wa chama hicho ambao hawakukamatwa, walihoji kwanini na wao hawakukamatwa. Wanasheria wa chama hicho akiwemo, Peter Kibatala, walionekana wakiingia na kutoka ndani ya kituo hicho, wakifanya mawasiliano na baadhi ya wabunge wao waliokusanyika nje ya Kituo cha Polisi Reli.
Ilipotimu saa 1:30 usiku viongozi
hao akiwemo Lowassa waliachiwa kwa dhamana na polisi baada ya kumaliza kuhojiwa. Juni 8, mwaka huu, polisi ilitangaza kupiga marufuku maandamano na
mikutano ya hadhara, iliyokuwa imepangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya siasa. Aidha, katazo hilo lilikwenda pamoja na lile lililotolewa wiki iliyopita la kupiga marufuku mikutano ya ndani ya kisiasa baada ya kubainika mikutano hiyo kutumika kuchochea vurugu
nchini.
Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya, alisema jeshi hilo limepokea taarifa kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa, vikitaka kufanya mikutano na maandamano, lakini wamepiga marufuku maandamano na mikutano hadi hapo
hali ya usalama itakapotengemaa.
“Vyama vingine vya siasa vimeonyesha dhamira ya kupinga kile ambacho kitasemwa na wapinzani wao,” alisema Mssanzya katika taarifa yake.
Taarifa hiyo ilisisitiza kuwepo kwa uwezekano wa kutokea vurugu baina ya makundi mawili ya kisiasa. Kutokana na hilo, aliwataka wanasiasa kuacha mara moja kushinikiza wananchi kutotii sheria za nchi.
Alisema polisi haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au
chama chochote kitakachokaidi agizo hilo.
Jeshi hilo pia, liliwataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kuvuruga amani ya nchi. Mbali na jeshi la polisi, viongozi wa dini, wasomi na baadhi ya wanasiasa nchini kwa nyakati tofauti wametahadharisha kufanyika kwa maandamano hayo kwa kuwa hayaashirihi kuwepo kwa utulivu.
Wakati huo huo,mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema amefi kishwa katika Mahakama ya Arusha na kusomewa mashitaka mawili.
Lema alifikishwa mahakamani hapo jana, mbele ya Hakimu Mkazi, Desideri Kamugisha na kusomewa shitaka la kutuma ujumbe wa kuudhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, unaosema ‘Karibu Arusha, tutakudhibiti kama Arabuni wanavyodhibiti mashoga’.
Shitaka la pili alilosomewa mbunge huyo ni kutuma ujumbe wa sauti kwenye mitandao ya kijamii, unaohamasisha maandamano yasiyokuwa na kibali.
Lema alikana mashitaka hayo na
Hakimu Mkazi, Kamugisha alimwachia huru kwa dhamana, ambapo katika shitaka la kwanza alidhaminiwa kwa sh. milioni 10 na shitaka la pili alidhaminiwa kwa sh. milioni 15.
Wakati akisubiri dhamana yake, Lema alizua taharuki baada ya kukataa kwenda magereza kabla ya muda wa mahakama kukamilika.

No comments:

Post a Comment