Thursday, 1 September 2016

HATUNA MUDA WA MAZUNGUMZO NA WANAOTAKA KUVUNJA AMANI-MASAUNI


SERIKALI imetoa onyo kali kuwa haitokubali kuona mtu au kundi lolote  linathubutu  kuchezea amani ya taifa na kwamba, ipo imara kuwalinda na kuwatetea wananchi kwa hali yoyote.

Aidha, imesema haina muda wa mazungumzo na mtu au kundi lolote, ambalo litautumia mgongo wa kudai demokrasia kwa lengo la kuleta machafuko.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad  Masauni, jijini Dar es Salaam, jana, wakati akizindua  programu ya  kidini ya Tunza  Amani Ikutunze, inayoendeshwa na Taasisi ya Peace Strengthen and Economic Derivative (PSEDO).

Masauni alisema wapo baadhi ya wanasiasa hapa nchini, ambao wanataka kukiuka sheria za nchi kwa kuhamasisha wananchi kuandamana na kufanya mikusanyiko kinyume cha sheria.

Alisema chombo chenye mamlaka kusimamia usalama wa wananchi na mali zao ni Jeshi la Polisi na linapotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa katiba na sheria hizo, kila mwananchi anawajibika kuliheshimu.

“Kwa mujibu wa  sheria ya vyama vya siasa, sehemu ya 11, inazungumzia utaratibu wa kufanya mikusanyiko na mikutano.
Vilevile sheria ya polisi ya mwaka 2012, inaeleza utekelezaji wa utaratibu huo,”alisema Masauni.

Aliongeza kuwa serikali  kupitia taarifa za kiintelijensia, iliamua kuzuia maandamano na mikutano ya kisiasa isiyo na tija katika wakati huu ili wananchi  waweze kushiriki  kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

“Wananchi wanataka kuungana na hatua za serikali, kupambana na wezi, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, miradi mbalimbali ya maendeleo, huduma za afya na elimu,”alisema Masauni.

Aliongeza: ”Hatutarajii mtu au kikundi  kiwahamasishe  wananchi kuvunja sheria za nchi na kukwamisha jitihada njema, ambazo serikali imekuwa ikifanya kwa nia ya kuwaondoa wananchi katika changamoto za umasikini.”

Masauni alisema serikali ipo imara kukabiliana na mtu ywyote, iwe leo au kesho, ambaye atathubutu  kuhamasisha wananchi kuandamana au kufanya mikutano isiyo na tija.

“Wito  wangu kwa  kwa wanasiasa, tutii mamlaka na sheria za nchi. Wananchi  wasikubali  kuhamasishwa kuvunja sheria za nchi yetu. Tutawashughulikia, iwe leo au kesho na siku yoyote,”alionya Masauni.

No comments:

Post a Comment