Thursday, 1 September 2016

VIGOGO SITA NIDA WAENDELEA KUSOTA RUMANDE

NA FURAHA OMARY

UPELELEZI wa kesi ya kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 1.16, inayowakabili vigogo wanane wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Dickson Maimu, haujakamilika.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai, akishirikiana na Wakili Fatuma Waziri, alidai hayo jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage.

Swai alidai shauri hilo lilipelekwa kwa kutajwa na kwamba, mshitakiwa wa kwanza (Maimu), hayupo na taarifa walizopata kutoka kwa Ofisa Magereza ni kwamba, ameshindwa kufika kwa kuwa ni mgonjwa.

Wakili huyo aliomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa. Hakimu Mwijage aliahirisha shauri hilo hadi Septemba 14, mwaka huu na kusema, dhamana za washitakiwa Meneja Biashara Avelin Momburi na Mkurugenzi wa Tehama, Joseph Makani zinaendelea.

Momburi na Makani waliachiwa kwa dhamana na Mahakama ya Kisutu kwa kuwa mahakama hiyo inayo mamlaka ya kuwapatia dhamana.

Hakimu Mwijage alisema washitakiwa Maimu na wenzake watano wataendelea kubaki rumande hadi tarehe hivyo.

Mbali na Maimu, washitakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao wanasota rumande kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kutoa dhamana ni Kaimu Mhasibu Mkuu wa NIDA, Benjamin Mwakatumbula.

Pia, wamo Mkurugenzi wa Kampuni ya Aste Insurance Brokers, Astery Ndege, Ofisa Usafirishaji, George Ntalima, Mkurugenzi wa Sheria, Sabina Raymond na Xavery Kayombo.

Washitakiwa hao sita wapo rumande kwa kuwa mahakama yenye mamlaka ya kuwapatia dhamana ni Mahakama Kuu, kutokana na mashitaka yanayowakabili kufunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na kiwango kinachohusika ni zaidi ya sh. milioni 10.

Katika kesi hiyo, Maimu na wenzake saba wanakabiliwa na  mashitaka 27, yakiwemo ya  kutumia madaraka vibaya, kutumia nyaraka za uongo kumdanganya mwajiri, kuisababisha NIDA hasara ya sh. 1,169,352,931 na kula njama.

Wakati huo huo, maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na Maimu na wenzake hao watano, ambao wapo rumande, yamepangwa kusikilizwa  kesho katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Maombi hayo yatasikilizwa mbele ya Jaji Eliezer Feleshi, baada ya upande wa jamhuri kuwasilisha hati kinzani ya majibu kuhusu maombi hayo.

Maimu, Mwakatumbula, Ndege, Ntalima, Sabina na Kayombo kwa kupitia mawakili wao, waliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu, wakidai kwamba mashitaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria na wana wadhamini wa kuaminika.

Maimu na wenzake hao waliwasilisha maombi hayo kwa  kupitia jopo la mawakili wanaowatetea katika kesi hiyo,  Michael  Ngalo, Seni Malimi, Audax Kahendaguza, Sylvester Kakobe, Gordian Njaala, Godwin  Nyaisa.

Kigogo huyo wa NIDA na wenzake, wamewasilisha maombi hayo yakiambatana na hati ya kiapo, muapaji akiwa Wakili Ngalo kwa niaba ya wenzake, ambapo wanaiomba Mahakama Kuu, kuwapatia dhamana kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria.

Aidha, wakili huyo anadai waleta maombi wana wadhamini wa kuaminika, ambao watahakikisha wanafika mahakamani wanapohitajika.

Pia, anadai waleta maombi walikamatwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Polisi na waliachiwa kwa dhamana, wana makazi Dar es Salaam na familia zao, ambazo zinawategemea na walionyesha ushirikiano kwa wapelelezi kuhusiana na mashitaka yanayowakabili.

No comments:

Post a Comment