Thursday 13 October 2016

JPM ACHUKUA UAMUZI MZITO, AWAPIGA MARUFUKU VIONGOZI WA SERIKALI KWENDA KUZIMA MWENGE SIMIYU, AWAAGIZA WALIOCHUKUA POSHO WAZIRUDISHE



RAIS Dk. Joh Magufuli ameagiza viongozi  wa serikali walioalikwa kuhudhuria sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, zitakazofanyika Bariadi mkoani Simiyu, kutohudhuria sherehe hizo na waliolipwa posho wazirejeshe.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi,  ilisema Rais Dk. Magufuli ametoa maagizo hayo, ikiwa ni utekelezaji wa azma ya serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali katika shughuli za maendeleo.

Ilisema viongozi waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na wakuu wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi wote wa mamlaka za serikali za mitaa, mameya na wenyeviti wote wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya.

Iliwataja wengine kuwa ni watumishi, ambao huambatana nao wakiwemo madereva na wasaidizi wao, ambao kwa idadi yao hufikia takribani 1,500.

Taarifa ya Ikulu ilifafanua kuwa, kwa kuwa sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru huambatana na maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Muasisi wa Taifa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, viongozi wote wa mikoa na wilaya wametakiwa kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.

Aidha, Rais Dk. Magufuli ameagiza wilaya zote, ambazo zimefanya vizuri katika shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao, zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha mbio za Mwenge na kwamba, zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa utaratibu utakaoelekezwa na mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.

Hata hivyo, Rais Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Taifa, viongozi wote wa serikali ya mkoa wa Simiyu, wilaya zake na wananchi wote wa mkoa huo, wajitokeze kwa wingi kushiriki katika sherehe za kuzima Mwenge, kesho.

Mgeni rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru, mwaka huu, atakuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment