Thursday 13 October 2016

TIKETI ZA DALADALA SASA KWA ELEKTRONIKI

MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imesema abiria wanaotumia usafiri wa daladala Dar es Salaam, wataanza kulipa nauli kwa mfumo wa kieletroniki, ifikapo Januari Mosi,  mwakani.

Aidha, ulipaji wa tiketi kwa mfumo wa kieletroniki umetajwa kuwa utasaidia kudhibiti udanganyifu na kuongeza mapato kwa serikali.

Uamuzi huo ulitangazwa jana, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Barabara wa SUMATRA,  Johansen Kahatano, katika uzinduzi wa kampeni ya usafi kwa madereva wa daladala na uvaaji wa sare.

Kahatano alisema ili kuhakikisha mfumo huo unafanikiwa, tayari mabasi 20, ya daladala yamefungiwa mfumo huo kwa majaribio.

Alisema kuwa mbali na mfumo huo kuongeza mapato, utasaidia kuondoa usumbufu wa kuongezeka kwa bei ya tiketi bila utaratibu maalumu na kusimamia haki za abiria, madereva na wamiliki.

Kahatano alisema kwa miaka mingi sasa, ajira ya udereva imekuwa haina heshima kutokana na kutokuwepo mifumo mizuri, hivyo hatua hiyo itasaidia kuwapo kwa ajira za uhakika kwa  kila dereva.

Pia, alizungumzia uvaaji sare za madereva na kutoa siku 14 kwa kila dereva kuwa nazo na hatua kali zitachukuliwa kwa atakayekaidi.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Awadh Haji, aliwaonya madereva wataokatisha safari na kusema atatoa dozi nzito kwao.

"Dereva yeyote asiye na sare ama anayekatisha safari, atawekwa mahabusu wakati utaratibu wa kupelekwa mahakamani ukifanyika,"alisema.

Aliongeza kuwa hawatakuwa na kicheko kwa yeyote atakayekiuka sheria ili kufanya jiji kuwa na nidhamu katika sekta ya usafiri na kusisitiza usafi kwa madereva na magari na kuheshimu kazi hiyo kama kazi nyingine.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa madereva, Shaban Mdemu,  alisema wakati umefika wa sekta ya udereva kutambuliwa rasmi kisheria.

Alisema hata wao wanaunga mkono mfumo huo wa kielektroniki kwa kuwa utafanya sekta hiyo kurasimishwa na kutambuliwa kisheria na madereva kupewa mikataba ya ajira na kuondokana na udereva kuwa ajira isiyo na heshima.

No comments:

Post a Comment