Thursday 13 October 2016

WATUMISHI SITA WATUMBULIWA TEMESA



MTENDAJI Mkuu wa TEMESA, Dk. Mussa Mgwatu amemuagiza Meneja wa Mwanza, Mhandisi Ferdinand Mishamo, kuwafuta kazi mara moja watumishi sita wa Kivuko cha Mv Kome.

Dk. Mgwatu alisema agizo hilo linapaswa kutekelezwa kuanzia jana na kuwapa onyo kali watumishi wengine wawili wa kivuko hicho kwa kuondoka katika eneo la kazi bila ruhusa ya mkuu wao wa kazi.

Alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha TEMESA mkoani Mwanza na kutembelea Kivuko cha Mv. Kome, kinachotoa huduma ya usafiri kati ya Kome na Nyakarilo, wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Dk. Mgwatu pia alimwagiza Meneja wa TEMESA Mwanza, Mishamo,  kuhakikisha wafanyakazi wa karakana na kivuko wanawajibika ipasavyo ili kuondokana na uzembe kama uliojitokeza.

“Hatuwezi kuvumilia uzembe namna hii. Watumishi wanaamua tu kuondoka eneo la kazi bila kupata ruhusa kutoka kwa wakuu wao, hii si sawa kabisa na nakuagiza hawa watumishi waachishe kazi mara moja,” alisisitiza Dk. Mgwatu.

Aidha, alimwagiza meneja huyo kuajiri watumishi wengine ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji.

Kwa upande wake, Mishamo alikiri kuwa hakukuwa na ruhusa yoyote ya maandishi iliyotolewa kwa  watumishi kutokuwepo kazini siku hiyo.

Aliwataja watumishi walioachishwa kazi kuwa ni walinzi wanne, Apolinary Kapulula, Marwa Nchagwa, Msomi Stanley na Joseph Mtokambali. Wengine ni Baharia Geofrey Biseko na mkusanya mapato wa kivuko hicho, Elisha Mbondo.

Mishamo aliwataja watumishi waliopewa onyo kali kuwa ni Mkuu wa Kivuko, Elias Mabushi na dereva wa kivuko hicho, Juma Bugingo.

No comments:

Post a Comment