NA SYLVIA SEBASTIAN
UPELELEZI wa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa macho Said Mrisho, inayomkabili Salum Njwete (34), maarufu kwa jina la Scorpion haujakamilika.
Scorpion, alipandishwa kizimbani jana, katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mbele ya Hakimu Adelf Sachore, wakati shauri hilo lilipopelekwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa Serikali, Munde Kalombora alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Sachore aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 19, mwaka huu, kwa kutajwa na mshitakiwa amerudishwa rumande kutokana na shauri linalomkabili kutokuwa na dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa ambaye ni mwalimu na mcheza karate, alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu, maeneo ya Buguruni Shell, wilayani Ilala.
Ilidaiwa mshitakiwa aliiba cheni ya silver yenye uzito wa gramu 38, ikiwa na thamani ya sh. 60,000, bangili, fedha taslimu sh. 331,000, pamoja na pochi, vyote vikiwa na thamani ya sh. 476,000, mali ya Said Mrisho.
Kabla na baada ya wizi huo, mtuhumiwa anadaiwa alimtishia mlalamikaji na kisha kumchoma kwa kisu machoni, tumboni na mabegani.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani hapo akiwa amevaa fulana nyekundu na suruali ya jeans, lakini alipotoka alikuwa amevaa shati na kofia kama zinazovaliwa na maustaadhi ili asitambuliwe.
Inasemekana kuwa, aliporudishwa mahabusu baada ya shauri hilo kuahirishwa, mshitakiwa huyo alibadili mavazi ili kuwazuga waandishi wa habari wasiweze kumbaini.
Akisimulia mkasa huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipomtembelea nyumbani kwake wiki iliyopita ili kumjulia hali, Mrisho alielezea jinsi alivyochomwa visu na kutobolewa macho hadi kupoteza uwezo wa kuona tena.
Alidai ilikuwa saa nne usiku, akitokea ofisini kwake Tabata, alipofika maeneo ya Buguruni Shell, aliona kuna wauza kuku na wafanyabiashara wengi waliokuwa wakimwita.
Alisema wakati anataka kununua kuku, alitoa sh. 32,000, akampa muuzaji sh. 11,000, ambapo alibaki na sh. 21,000, kwenye upande mmoja wa mifuko yake ya suruali huku upande mwingine akiwa na fedha zingine zilizokuwa kwenye pochi.
"Nilikuwa nimesimama muda huo, akatokea mtu akasimama upande wa kulia kwangu, akaniambia ‘bro nina shida’. Nikamwambia ‘bro ongea shida yako kabla sijatoka hapa maana nikitoka hapa sina mtu wa kumsikiliza kwa sababu Buguruni sina ninayemjua, halafu huwa sina kawaida ya kuja Buguruni'," alisimulia.
“Nikashtukia napigwa kisu cha bega la kushoto cha haraka haraka, nikapigwa mgongoni, nikapigwa begani tena, nikapiga kelele ‘jamani nisaidieni mwizi’ kwa sababu nilijua atakuwa ni mwizi. Akanipiga kisu cha tumbo, anachoma halafu anakata, anachoma halafu anainua kisu, akanipiga visu vya haraka haraka kama saba,’’alidai Mrisho.
Alisema hakuna mtu aliyeshikwa na butwaa wakati alipokuwa akifanyiwa ukatili huo na kwamba, alipopigwa kisu cha tumbo, hakuna aliyekuwa akistuka wala kumtetea, ingawa kulikuwa na wauza kuku zaidi ya 40.
"Baada ya kunipiga visu sehemu mbalimbali za mwili, alinipeleka barabarani ili nigongwe na gari, apoteze ushahidi, lakini aliona gari zinanipita, akanitoboa macho, akawa bado hajaondoka na watu wanamuangalia.
"Akishakupeleka barabarani, anataka ugongwe na gari apoteze ushahidi. Alivyonivutia barabarani, hapo tayari alikuwa ameshawaondolea ushahidi wauza kuku pale ili siku nyingine mtu yeyote akija asijue,"alisema.
No comments:
Post a Comment