Wednesday, 16 November 2016
MPEMBA WA MENO YA TEMBO KIZIMBANI
NA FURAHA OMARY
MTUHUMIWA Yusuf Ali Yusuf, maarufu kama Mpemba na wenzake watano, wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa kukusanya na kuuza meno ya tembo, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Mpemba na wenzake, walifikishwa mahakamani hapo jana, ambapo walisomewa mashitaka manne ya kujihusisha na biashara ya vipande 50, vya meno ya tembo vyenye thamani ya sh. 392,817,600.
Mbali na Mpemba, ambaye kwa jina lingine anajulikana kama Shehe (35), ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam, washitakiwa wengine ni mfanyabiashara Charles Mrutu au Mangi Mapikipiki au Mangi (37), mkazi wa Mlimba, Morogoro.
Pia, wamo wafanyabiashara Benedict Kungwa (40), mkazi wa Mbagala Chamazi, Dar es Salaam, Jumanne Chima (30) au Jizzo au JK, mkazi wa Mbezi Msakuzi, dereva Ahmed Nyagongo (33), mkazi wa Vikindu, Mkuranga na mfanyabiashara Pius Kulagwa (46), mkazi wa Temeke.
Mpemba na wenzake walifikishwa mahakamani hapo mapema asubuhi na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Wakili wa Serikali, Paul Kadushi akishirikiana na Elia Athanas, aliwasomea washitakiwa hao mashitaka manne ya kujihusisha na mtandao wa uhalifu na kukutwa na nyara za serikali, ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo.
Akiwasomea mashitaka, Kadushi alidai tarehe tofauti kati ya Januari 2014 na Oktoba, mwaka huu, sehemu tofauti katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Tanga na Mtwara, washitakiwa kwa pamoja na wengine, ambao hawajafikishwa mahakamani, kwa makusudi waliendeleza mtandao wa uhalifu.
Alidai washitakiwa hao walikusanya na kuuza nyara za serikali, ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 (sawa na sh. 392,817,600), mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Pia, washitakiwa hao wanadaiwa Oktoba 26, mwaka huu, maeneo ya Mbagala Zakhem, wilayani Temeke, Dar es Salaam, walikutwa na nyara za serikali, ambazo ni vipande 10, vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85, vikiwa na thamani ya Dola za Marekani 30,000 (sawa na sh. 65,469,600), mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Shitaka la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Oktoba 27, mwaka huu, maeneo ya Tabata Kisukulu, wilayani Ilala, Dar es Salaam, walikutwa na vipande vinne vya meno hayo, vikiwa na uzito wa kilo 11.1, vyenye thamani ya Dola za Marekani 15,000 (sawa na sh.32,734,800), mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Aidha, washitakiwa wanadaiwa Oktoba 29, mwaka huu, eneo la Tabata Kisukulu, walikutwa na vipande 36, vya meno hayo, vikiwa na uzito wa kilo 58.55, vyenye thamani ya Dola za Marekani 135,000 (sawa n ash. 294,613,200), mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la uhujumu uchumi.
Wakili Kadushi aliitaarifu mahakama kwamba, upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wako katika maandalizi ya kuchapa maelezo ya mashahidi na vielelezo ili waweze kupeleka taarifa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Kutokana na hilo, Kadushi aliomba kupewa tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo wakati wakiendelea na taratibu hizo.
Kwa upande wa washitakiwa, ambao hawakuwa na mawakili wanaowawakilisha, Mpemba alidai ana matatizo ya kiafya kutokana na kipigo alichokipata siku alipokamatwa.
Alidai alipigwa sana, kiasi kwamba kichwa kinamuuma na anasikia kizunguzungu na masikio hayasikii vizuri, hivyo aliomba mahakama impatie fomu namba tatu ya matibabu (PF3).
Mshitakiwa Mangi, naye aliiomba mahakama kumpatia fomu hiyo ili aweze kwenda kutibiwa kwa madai ameumizwa kidole kwani kucha imetoka na sikio linatoa usaha.
Maombi ya kupatiwa fomu hiyo kwa ajili ya matibabu yalitolewa pia na washitakiwa wengine, ambao walidai kupigwa.
Baada ya kusikiliza maombi hayo, Hakimu Simba aliwataarifu washitakiwa hao kwamba, matibabu watapatiwa na Jeshi la Magereza kwa kuwa wanapelekwa gerezani, ambako kuna utaratibu wa kutoa matibabu.
Hakimu aliwaambia washitakiwa hao kwamba, mahakama haitoi fomu hiyo na haiwezi kutoa amri yoyote na kuahirisha shauri hilo hadi Desemba mosi, mwaka huu, litakapopelekwa kwa kutajwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment