POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, imewakamata wanawake wanne na watoto wanne, waliokuwa wamefichwa katika Pori la Vikindu mkoani Pwani.
Taarifa zilizotolewa na polisi zinaeleza kuwa, watoto hao walikuwa wakifundishwa uhalifu wa kutumia silaha katika matukio ya kigaidi.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema mafanikio ya kuwapata wanawake na watoto hao, yametokana na kikosi maalumu
kufanya operesheni kali katika maeneo mbalimbali ya pori hilo na kuwakamata watoto wanne, waliotoroshwa katika familia ya Abdala Maleck.
Watoto hao, ambao majina yao yanahifadhiwa, walipatikana baada ya mzazi mmoja wa kiume, aliyejulikana kwa jina la Shabani Abdala Maleck, mkazi wa Kitunda, kutoa taarifa polisi ya kutoroshwa kwa watoto hao na mtalaka wake, aitwaye Salma Mohamed, aliyeingizwa kwenye harakati hizo za kigaidi.
Aidha, alisema jitihada za pamoja kati ya mtoa taarifa na polisi ziliweza kufanikisha kuwakamata wanawake na watoto hao katika eneo la Kilongoni, Vikindu mkoani Pwani.
Kamanda Sirro alisema watoto hao walikuwa wamekusanywa kwenye nyumba ya mtu mmoja, anayeitwa Suleiman, wakiwa wanafundishwa mambo ya dini na harakati za ugaidi.
“Watoto hao ni wanafunzi wa shule ya msingi Kizange na Jitihada, zilizoko maeneo ya Kitunda, mmoja akiwa darasa la saba (13), wawili darasa la nne na mmoja mdogo akiwa na umri wa miaka miwili.
“Baada ya mahojiano zaidi, imeijidhihirisha kuwa wengi wao wameachishwa masomo katika shule mbalimbali nchini, ambapo baadhi ya watoto wameachishwa na wazazi, walezi wao na kuingizwa katika madrasa, ambazo ndizo kambi walikokamatiwa chini ya uangalizi wa wanawake waliokamatwa nao,” alisema.
Sambamba na mafunzo ya madrasa, pia wamekuwa wakifundishwa ukakamavu (karate, kungfu, judo) na silaha aina ya SMG na bastola.
Pia, wanafundishwa kupiga maeneo tete ya kummaliza mtu pumzi na kufariki haraka wakati wa mapigano (pressure point) ili kumdhibiti adui.
Aidha, alisema watoto hao wamefundishwa jinsi ya kulenga shabaha kwa kutumia risasi, kutumia kitako cha bunduki na singe na kwamba, adui yao mkubwa ni polisi, walinzi katika taasisi za fedha na makafiri katika kujipatia kipato. Pia alisema wamefunzwa kupora au kunyang’anya kwa kutumia silaha na kutumia viungo vyao.
Kamanda Sirro alisema wanawake hao na watoto wanaendelea kushikiliwa kwa ajili ya mahojiano ili kuweza kubaini mtandao mzima katika suala hilo kwa lengo la kutokomeza tabia hiyo ya kuwaachisha watoto wadogo shule na kuwaingiza katika vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo, polisi imesema itajitahidi kuhakikisha watoto hao wanawarudisha kwa wazazi wao ili waendelee na masomo yao.
Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kutengua mbinu mpya ya wakwepa kodi, inayotumiwa na wakazi wa Mbweni ili kupitisha bidhaa zisizolipiwa ushuru.
Kamanda Sirro alisema mbinu hizo zimekuwa zikitumika katika njia wanazotumia kupitisha bidhaa zisizolipiwa ushuru, ambapo wanatega mbao zenye misumari, nia yao ikiwa ni kuharibu magari ya doria.
Alisema watu hao wamekuwa wakitandika mbao hizo chini ya barabara ili magari ya polisi na TRA yapate pancha na kushindwa kuwafuatilia.
Kamishna Sirro ametoa onyo kali kwa wananchi wa maeneo hayo, akisema operesheni kali inaendelea ili kuwakamata wote wanaofanya vitendo hivyo na sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Kamanda Sirro alisema jeshi hilo limefanikiwa kukamata magari manne yaliyoibiwa na watuhumiwa wanne, akiwemo Padri wa Kanisa Katoliki Sumbawanga, Demestious Apolinary.
Watuhumiwa wengine ni Amani Dickson (23), mkazi wa Kigamboni, Exaud Martin (40), mkazi wa Mikocheni, Rashid Haruna (28) na Mzee Nassibu(41), mkazi wa Yombo.
Hata hivyo, Sirro alisema upelelezi bado unaendelea ili kubaini iwapo mali hizo wamezipata katika mazingira yapi na ukikamilika watafikishwa mahakamani.
No comments:
Post a Comment