Wednesday, 16 November 2016

LEMA AENDELEA KUSOTA RUMANDE


NA LILIAN JOEL, ARUSHA

MAWAKILI wanaomtetea mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), anayesota rumande katika Gereza la Kisongo, wamewasilisha barua ya maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, wakiiomba iitishe mafaili ya kesi za uchochezi zinazomkabili mbunge huyo.

Lema, kwa kupitia mawakili wake, Peter Kibatala na Shack Mfinanga, wamewasilisha barua hiyo mahakamani hapo na kupelekwa kwa Kaimu Jaji Mfawidhi, Sekela Moshi, ambapo bado majibu yanajatolewa ya kukubaliwa maombi yao ama la.

Mawakili hao wamedai kwamba, wameamua kuwasilisha barua hiyo kwa kuwa wanaamini kuna makosa ya kisheria yaliyofanywa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kwa lengo la kumnyima dhamana mbunge huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, nje ya viunga vya mahakama hiyo, Wakili Mfinanga, alidai wameamua kuwasilisha barua hiyo ili mahakama iitishe mafaili hayo na kujua ni kwanini Lema amekosa dhamana, ambayo awali Hakimu Desdery Kamugisha alisema ipo wazi.

Alidai maombi hayo wameyawasilisha na kupokelewa na msajili huyo, hivyo wanasubiri kupangiwa jaji wa kuyasikiliza.

Wakili huyo alidai kuwa wameamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu  hawakuridhishwa na hatua ya Hakimu Kamugisha, kuruhusu dhamana, lakini kabla hajatoa masharti ya dhamana, mawakili wa serikali akiwemo Paul Kadushi, walikataa Lema kudhaminiwa na kusema wameonyesha nia ya kukata rufani.

"Tunapinga Lema kunyimwa dhamana iliyo wazi na ndio maana tumewasilisha maombi mahakama kuu ili iweze kuitisha mafaili na jaji atoe uamuzi juu ya kesi hizi," alidai.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi ya dhamana, mawakili wa serikali wakiongozwa na Kadushi, walipinga Lema kupewa dhamana kwa madai amefanya kosa akiwa amepewa dhamana na mahakama hiyo.

Pia, walidai iwapo Lema atapewa dhamana, kuna hatari ya usalama wa maisha yake.

Hata hivyo, Hakimu Kamugisha alisema mahakama haitoi dhamana kama hisani bali ni haki ya msingi ya mtuhumiwa kama ilivyoainishwa katika Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.

Alisema iwapo mtuhumiwa ananyimwa dhamana, sheria inatakiwa kutamka bayana.

“Sheria inakataza kufinyafinya uhuru wa mtuhumiwa kupata dhamana, lakini kama inabidi kumnyima dhamana, ni lazima yawepo mazingira na taratibu zilizoanishwa kisheria.

“Nimeshindwa kupata kifungu chochote cha sheria kinachomnyima mshtakiwa dhamana akiwa chini ya dhamana,” alisema.

Alisema katika kesi hiyo namba 440 na 441 ya mwaka huu, ambazo ziliunganishwa na kuwa shauri moja, mahakama hiyo haikutoa masharti yoyote kwa mshitakiwa (Lema) asipewa dhamana iwapo atakiuka dhamana.

Kuhusu usalama wa mtuhumiwa, alisema upande wa mashitaka umeshindwa kuonyesha namna mshitakiwa atakavyodhurika iwapo atapewa dhamana.

Aidha, alisema hakuna ukubwa wa tishio la usalama wa mshitakiwa, ambao polisi wameonyesha kuwa watashindwa kuuzuia.

“Nimeombwa nizuie dhamana, sijaona kifungu chochote cha sheria kufanya hivyo. Maamuzi ya pingamizi dhidi ya mshitakiwa halikuwa na sababu ya msingi, ninalitupilia mbali kwa kumpa dhamana kwa misingi ya  masharti nitakayotaja,” alisema.

Hata hivyo, kabla hakimu hajatoa masharti ya dhamana,  Kadushi, alisimama na kuwasilisha nia ya kukata rufani kupinga utekelezaji wa uamuzi huo, akitumia kifungu cha 379(1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kama ilivyofanyiwa marekebisho, ambapo alisema wanapinga Lema kupewa dhamana, hali iliyosababisha mbunge huyo kwenda mahabusu katika Gereza la Kisongo, Jijini Arusha hadi sasa.

Wakati huo huo, upande wa Jamhuri leo, unatarajia kuwasomea maelezo ya awali, Lema na mkewe Neema Godbless, wanaokabiliwa na kesi ya kumtukana Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Washitakiwa hao watapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Agustino Rwizile, baada ya kushindikana jana, kuwasomea maelezo hayo kutokana na Lema kutoletwa mahakamani.

Jana,  saa 2;32 asubuhi,  basi la Magereza lenye namba za usajili MT 0040, lilifika mahakamani hapo na kushusha mahabusu, lakini Lema hakuwepo, hali iliyomlazimu wakili wake, Mfinanga kumuuliza mmoja wa askari hao kwanini mteja wake hajaletwa mahakamani wakati anayo kesi ya kujibu.

Askari magereza huyo, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, alimjulisha wakili Mfinanga kuwa, magereza hawakupatiwa hati ya kumpeleka Lema mahakamani hapo.

Baada ya saa moja, shauri hilo liliitwa mbele ya Hakimu Rwizile, ambapo Wakili wa Serikali, Ali Mhalila, aliileza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Baada ya hoja hiyo, Wakili wa Utetezi, John Malya, aliieleza mahakama kuwa, wakili wa serikali amepitiwa na kwamba,  kesi hiyo  imekuja mahakamani hapo kwa ajili ya usikilizwaji wa hoja za awali na kwamba, anaomba mteja wake aletwe mahakamani ili aweze kusomewa hoja hizo kwani bado yuko gerezani .

Kutokana na majibu hayo, wakili wa serikali aliileza mahakama kwa kuwa mawakili wawili wa mtuhumiwa wapo mahakamnai hapo, kesi hiyo inaweza kuendelea kwani haitaathiri jambo lolote na kwamba, ilikuwa ni wajibu wa upande wa utetezi kujua kama mteja wao ameletwa mahakamani au laa.

Hata hivyo, Wakili Malya alipinga hoja hiyo na kuieleza mahakama kuwa, siyo wajibu wake kufanya hivyo na kwamba, ulikuwa wajibu wa upende wa Jamuhuri kwani wao ndiyo walipinga dhamana ya lema katika kesi namba 440 na 441, ambazo zimesababisha mteja wake kuwepo gerezani.

“Mheshimiwa hakimu, wakili wa utetezi asiitupie Jamhuri mpira huo, kwani ulikuwa ni wajibu wao kujua kama mshitakiwa ameletwa mahakamani au la, pia suala la mshitakiwa kuhudhuria mahakamni ni la mshitakiwa mwenyewe, siyo vinginevyo,” alisema.

Baada ya mabishano hayo yaliyomalizika saa  4.38,  hakimu aliahirisha kesi hiyo kwa muda na kuagiza Lema akachukuliwe gerezani ili apelekwe mahakamani hapo kusomewa hoja za awali.

Baada ya maelezo hayo, kesi iliahirishwa mpaka saa 6.50, ambapo iyo ilianza tena kwa mwanasheria wa serikali, kuieleza  mahakama kuwa, jitihada za kumleta Lema mahakamni hapo zilikwama kutokana na sababu zisizozuilika.

Kufuatia majibu hayo, Wakili Malya aliiomba mahakama imtake wakili wa Jamhuri kuleza ni sababu gani wanadharau amri ya mahakama na kumuomba hakimu kutoa adhabu kwa kuwa sheria iko wazi.

Aidha, wakili wa serikali aliieleza mahakama kuwa amri hiyo ilikuwa imetolewa kwa mafreza na siyo kwa mwanasheria wa serikali na kwamba, amepata taarifa kuwa magereza wamekosa gari kwa wakati huo la kumleta Lema mahakamani hapo.

Baada ya majibu ya hakimu, alimtaka karani wa mahakama kuandika hati nyingine ya kumtaka Wakili wa Serikali, kuhakikisha Lema anafikishwa mahakamni hapo leo, ili wasomewe maelezo ya awali.

Katika hatua nyingine, Hakimu Rwizile aliwataka polisi pamoja na askari magereza wanaokuja mahamani hapo, kuacha mara moja tabia ya kuwabughudhi waandishi wa habari wanaofika mahakamani hapo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao.

Rwizile alitoa agizo hilo jana, kutokana na waandishi wa habari kubughudhiwa mara kwa mara kwa kufukuzwa katika eneo la viwanja vya mahakama, pamoja na kuzuiliwa kuingia kwenye kesi mbalimbali  licha ya kuwa na vitambulisho pamoja na kibali cha mahakama cha kufanya kazi mahakamani hapo.

“Siyo lazima mje kuomba kibali kila siku mahakamani hapa  kwa ajili ya kutimiza wajibu wenu, mahakama ni mhimili unaojitegemea, hakuna mtu mwenye mamlaka ya kuwazuia kufanya kazi zenu, kuanzia sasa askari yeyote atakayewabughudhi katika eneo la mahakama, naomba mnipigie simu ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake,” alisema.

Kwa mujibu wa Rwizile, hakuna maelekezo yeyote yaliyotolewa na mahakama ya kuwakataza waandishi wa habari kuingia mahakamani hapo kwa ajili ya kutimiza wajibu wao na kwamba, kila mtu ana haki ya kuja mahakamani na kusikiliza kesi.

Leo, waandishi wa habari waliofika katika mahakama hiyo  walifukuzwa na polisi pamoja na askari magereza, ikiwa ni pamoja na kuzuia waandishi kuingia na magari yao mahakamni hapo bila ya sababu za msingi, pamoja na kuwatolea lugha chafu  na vitisho vya kuwajeruhi pamoja na  kuharibu magari yao.

No comments:

Post a Comment