Tuesday, 15 November 2016
NACTE YAVIFUTIA USAJILI VYUO 26
BARAZA la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), limevifutia usajili vyuo 26, kwa kushindwa kufuata taratibu za usajili, ambapo vyuo 20 vimekuwa vikiendesha mafunzo bila ya kibali.
Aidha, vyuo viwili vimekuwa vikiendesha mafunzo katika vituo visivyosajiliwa na baraza hilo.
Baraza hilo limewagiza wamiliki wa vyuo hivyo, kuwatafutia wanafunzi wenye sifa vyuo vingine ama kuwarejeshea ada zao.
Kaimu Katibu Mkuu wa NACTE, Dk. Adolf Rutayunga, alitangaza uamuzi huo jana, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dar es es Salaam.
Alisema wamevichukulia hatua vyuo hivyo kwa kuvifutia usajili kutokana na kushindwa kuzingatia kanuni za usajili wa baraza hilo.
Dk. Rutayunga alivitaja vyuo hivyo kuwa ni Institute of Managemment and Development Studies (Iringa), Green Hill Instute (Mbeya), Institute of Business and Social Studies (Mbeya), Royal College of Africa (Mbeya), Mbeya Training College, Mbengwenya College of Bussness and Information Technology (Mbinga).
Vyuo vingine ni New Focus College (Mbeya), Shukrani International College of Busness and Administration (Mbeya), Majority Teachers College, Rukwa College of Health Sciences (Sumbawanga), Litembo Health Laboratory Science School (Mbinga).
Pia vipo MAM Institute of Education (Mbeya), Belvedere Busness and Technology College (Mwanza), Geita Medical Laboratory Sciences and Nursing Training College (Geita), Muleba Academy Institute (Muleba), St. Benard Health Training Institute (Geita), Victoria Institute of Tourism and Hotel Management (Mwanza) na Gisan Institute of Health Science (Mwanza).
Kaimu Katibu Mkuu huyo aliongeza kuwa, vyuo vingine ambavyo vimekumbwa na sakata hilo ni Dar es Saalam Institute of Business Studies na Ellys Institute of Technology (Mara).
Vingine ni Tanzania Institute of Charted Secretaries and Administrators (Arusha), Emmanuel Community Institute (Kibaha), Modern Commercial Institute (Dar es Saalam) na Marian College of Law (Dar es Saalam).
Mbali na vyuo hivyo, Dk. Rutayunga alivitaja vyuo vingine, ambavyo vimekuwa vikiendesha mafunzo, ambayo hayajaidhinishwa na baraza hilo kuwa ni Dar es Salaan Institute of Journalism and Mass Communication vya Mwanza, Bukoba, Geita na Kahama.
Vyuo vingine ni The Golden Training Institute Dar es Salaam (kozi ya Certificate in Sales and Marketing, Certificate in Record Management and Certificate in Nursery Teachers), Early Childhood Education na National Institute of Agriculture (Arusha).
Dk. Rutayuga alivitaja vyuo vingine kuwa ni Musoma Utalii Training College (Musoma), Mwanza Polytechnic cha Mwanza na Maswa na Nkurumah Mkoba Teachers College, kilichoko Kongwa mkoani Dodoma.
Alisema NACTE imevibaini vyuo viwili vinavyoendesha mafunzo katika vituo, ambavyo havijapata kibali kuwa ni Mufindi Teachers College na Rungembwa Teachers College, vyote vya Mafinga.
Hivyo NACTE imewataka wamiliki wa vyuo, ambavyo havijakidhi masharti, kuhakikisha wanawatafutia vyuo vingine wanafunzi walio na sifa au kuwarudishia ada zao.
“Kwa wanafunzi wasio na sifa, walioko katika vyuo hivyo, mnapaswa kuwarudishia ada zao au kuwapeleka shule zinazowahusu,” alisisitiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment