Monday, 22 May 2017

WATUMISHI WATANO HALMASHAURI YA IGUNGA WATUMBULIWA


WATUMISHI watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, wamefukuzwa kazi na Baraza la Madiwani la halmashauri hiyo kwa makosa mbalimbali, ikiwemo wizi wa fedha.

Mkurugenzi  Mtendaji wa  halmashauri hiyo, Revocatus Kuuli, alisema hayo mwishoni mwa wiki, alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa, kuhusu kufukuzwa kazi kwa watumishi hao.

Aliwataja watumishi hao, nafasi zao zikiwa kwenye mabano kuwa ni Daudi Magembe (mlinzi), Nasibu Ngoitanile (tabibu msaidizi), Revocatus Msaku,  (ofisa mtendaji wa kijiji), Emmanuel Andrew (ofisa mtendaji kata) na Kizito William (dereva).

Alisema watumishi hao walifukuzwa kazi na baraza hilo Mei 12, mwaka huu, kwa makosa mbalimbali, ikiwemo wizi wa fedha, utoro, ulevi na kuisababishia halmashauri hasara.

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema pamoja na kuwaonya mara kwa mara watumishi hao, wameshindwa kubadilika, jambo ambalo madiwani walisema hawako tayari kuendelea nao katika halmashauri hiyo.

Kuuli alitoa wito kwa watumishi wanaopenda kufanyakazi kwa mazoea, kuacha mara moja kwani mtumishi yeyote atakayeshindwa kuendana na kasi ya awamu ya tano, hawatamvumilia.

Baadhi ya watumishi waliofukuzwa kazi, walidai uamuzi uliofanywa na madiwani hawawezi kuupinga, hivyo watatafuta kazi zingine za kufanya ili waweze kutunza familia zao.

No comments:

Post a Comment