Thursday, 6 July 2017
KABUDI: MIKATABA ILIYOPO YA MWISHO
SERIKALI imesema mikataba iliyopo ya madini ni ya mwisho na kuanzia sasa, wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika sekta hiyo watatumia leseni.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mjadala wa muswada wa sheria ya mabadiliko ya sheria mbalimbali ya mwaka 2017, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema sheria hiyo mpya ikitiwa saini, itabadilisha mfumo huo kutoka kwenye mikataba na kuwa mfumo wa leseni.
“Tutafanya marejeo ya mikataba iliyopo, itatolewa taarifa ya mapitio hayo kwa Bunge, sasa ungeendelea na mikataba ina maana tungekuwa tumevunja hiyo mikataba.
“Tunasema njooni kwa majadiliano na niseme hii ndiyo mikataba ya mwisho. Sheria hii ikipita, hakuna tena mikataba na hakuna leseni, hakuna mwekezaji ambaye atakuja baada ya sheria hii kwa makubaliano wote watakuwa ni leseni."
Alisema sheria iliyopita ilikuwa inataka mapitio ya mikataba ifanyike kila baada ya miaka mitano, lakini sasa baada ya makubaliano kuingiwa, Bunge linaweza kuipitia kila linapoona inafaa.
“Baada ya kuingia makubaliano, taarifa zitapelekwa bungeni katika kikao cha Bunge linalofuata, ndiyo maana tumeondoa miaka mitano na itafanywa kwa jinsi Bunge litakavyoagiza, hata ikiwa ni baada ya mwaka mmoja. Kama Bunge litaona kuna kifungu hakipo kwa maslahi ya umma hatusubiri miaka mitano,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema kuwa na kipengele cha kupitia mikataba ya madini kwenye sheria ya madini hakikua na nguvu ya sheria ambayo ingesaidia kuwabana wawekezaji.
Alisema serikali itaufanyia kazi ushauri wa Zitto Kabwe (Kigoma Mjini - ACT Wazalendo) aliyependekeza serikali kwenda na mfumo 'production sharing' kama ilivyo sheria za petroli, badala ya mfumo wa sasa wa 'development sharing'.
Alisema kwa sasa wameamua kuwa na mfumo wa serikali kuwa na hisa ambazo hazitafifiswa kwenye mtaji kenye migodi ambayo si chini ya asilimia 16 ambazo hazitafifishwa na kuwa na uwezo wa kuongeza hisa hadi kufikia asilimia 50.
“Kwenye mambo kama haya yanayohusu taifa, tunapaswa kuwa wamoja, hivi kuna ubaya gani kuhusu sheria tulizoleta za kusimamia maliasili zetu kwa manufaa ya taifa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge Job Ndugai ameunda Kamati maalum ya ushauri kuhusu mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini, yenye wajumbe tisa ikiongozwa na Mussa Azzan Zungu.
Akizungumza kabla ya kuhitimisha shughuli za Bunge la Bajeti jana Spika , Ndugai alisema ameunda kamati hiyo kupitia Waraka wa Spika namba 3 wa mwaka huu.
Ndugai alisema kazi ya kamati hiyo ni pamoja na kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini, kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri serikali kuhusiana na uendeshaji bora wa biashara ya madini hayo nchini.
Spika aliwataja wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Dk. Immaculate Semes (viti maalumu - CHADEMA) Shally Raymond (viti maalumu - CCM) Rashid Ali Abdallah (Tumbe - CUF) Allan Kiula (Iramba Mashariki - CCM) Restituta Mbogo (viti maalumu - CCM) Ahmed Juma Ngwali (Wawi - CUF).
Wengine ni Richard Ndassa (Sumve - CCM) Emmanuel Mwakasaka (Tabora Mjini - CCM).
Spika alisema kuundwa kwa kamati hiyo ni hatua mojawapo ya utekelezaji wa Azimio la Bunge la kumpongeza Rais Dj. John Magufuli katika jitihada za kulinda rasilimali za taifa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment