MAHAKAMA
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana ilihamia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, kumsomea mashitaka ya kesi ya uhujumu
uchumi, mfanyabiashara Yusuf Manji, akiwa amelazwa.
Kutokana
na hatua hiyo, washitakiwa wenzake watatu ambao ni wafanyakazi wake, akiwemo
Meneja Rasilimali Watu, Deogratius Kisinda, ililazimu wapelekwe hospitalini
hapo ili wasomewe mashitaka pamoja na bosi wao.
Manji
na wenzake walisomewa mashitaka saba yakiwemo ya kukutwa na vitambaa
vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na mihuri
ya JWTZ, ambayo yanaangukia chini ya sheria za uhujumu uchumi na usalama wa taifa.
Kufuatia
mashitaka hayo, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), aliwasilisha hati ya
kupinga dhamana kwa watuhumiwa hao.
Mbali
na Manji (41) na Kisinda (28), washitakiwa wengine ni mtunza stoo Abdallah
Sangey (46), mkazi wa Jangwani na mtunza stoo msaidizi Thobias Fwele (43),
mkazi wa Chanika.
Mahakama
hiyo ilianza safari ya kuhamia hospitalini hapo saa 8.30 mchana, ambapo ilipofika
saa 9.10 alasiri, maofisa wa mahakama,
wakiwemo mawakili wa serikali na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma
Shaidi na mawakili wa washitakiwa hao, walifika hospitalini hapo.
Msafara
huo, ulielekea hadi katika ghorofa ya pili ya jengo la taasisi hiyo, kwenye
wodi namba moja, ambapo upande wa jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali
Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi, akishirikiana na Mawakili wa Serikali
Waandamizi, Nassoro Katuga na Tulumanywa Majigo, uliwasomea washitakiwa hao
mashitaka hayo.
Manji
akiwa kitandani huku ametundikiwa dripu, akiwa amevalia nguo za wagonjwa na
wenzake wakiwa pembezoni mwa kitanda chake, walisomewa mashitaka ya kujipatia
bidhaa isivyo halali, kukutwa na mihuri ya serikali isiyo halali na kukutwa na
mali inayodhaniwa imepatikana isivyo halali.
Katika
mashitaka hayo, Manji na wenzake wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, maeneo ya
Chang’ombe ‘A’, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kwa pamoja walikutwa na ofisa
wa polisi wakiwa na mabando 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za
JWTZ, zenye thamani ya sh. milioni 192.5 ambavyo vilipatikana isivyo halali.
Pia,
washitakiwa hao wanadaiwa Julai Mosi, mwaka huu, katika maeneo hayo, walikutwa
na ofisa wa polisi, wakiwa na mabando manane ya vitambaa hivyo, vyenye thamani
ya sh. milioni 44.
Shitaka
la tatu, washitakiwa hao wanadaiwa Juni 30, mwaka huu, katika eneo hilo,
walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maandishi “MKUU WA KIKOSI 121 KIKOSI CHA JESHI
JWTZ”, bila ya kuwa na uhalali kitengo
ambacho kingeweza kuhatarisha usalama wa nchi.
Washitakiwa
hao wanadaiwa siku hiyo, walikutwa na mhuri wa JWTZ wenye maneno “KAMANDA
KIKOSI 834 KJ MAKUTUPORA DODOMA,” bila ya kuwa na uhalali, kitendo ambacho
kingeweza kuhatarisha usalama wan chi.
Manji
na wenzake, pia wanadaiwa siku hiyo walikutwa na mhuri mwingine wenye maneno
COMANDING OFFICER 835 KJ, MGAMBO P.O BOX 224 KOROGWE.
Washitakiwa
hao wanadaiwa Julai Mosi, mwaka huu, katika eneo hilo, walikutwa na vibao vya
namba za usajili za magari vyenye namba SU 383 na SM 8573 ambavyo vilipatikana
isivyo halali.
Mapema
wakati mashitaka yanaanza kusomwa, Manji alikuwa amekaa kitandani, lakini
baadaye alilala na kujifunika blanketi na kuendelea kusikiliza mashitaka yake.
Baada
ya washitakiwa hao wanaotetewa na mawakili Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na
Seni Malimi, kusomewa mashitaka, hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama
hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa sababu wameshitakiwa chini ya sheria
za uhujumu uchumi na usalama wa taifa.
DPP
AWASILISHA HATI YA KUPINGA DHAMANA
Upande
wa jamhuri uliwasilisha hati ya kupinga dhamana kutoka kwa DPP, akiomba
washitakiwa wasiruhusiwe kupewa dhamana.
Mawakili
hao wa serikali, walidai DPP anaona washitakiwa wakiachiwa kwa dhamana
watahatarisha usalama na maslahi ya nchi na kwa mujibu wa shitaka la kwanza na
la pili, Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kushughulikia suala la dhamana.
MAWAKILI
WA MANJI WAPINGA HATI YA DPP
Kwa
upande wa mawakili wa washitakiwa hao, walipinga wateja wao kuzuiwa wasipewe
dhamana kwa vile mashitaka namna yalivyo, yanaiondolea mahakama hiyo kufikiria
suala la dhamana lakini kwa nia mbaya iliyoonyeshwa na upande wa jamhuri.
“Upande
wa jamhuri umewasilisha hati ya DPP kupinga dhamana, kitendo ambacho tunaona
kama ni matumizi mabaya ya madaraka na hakitendi haki kwa washitakiwa,” walidai
mawakili hao.
Ndusyepo
alidai jana Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi namba
115 ya mwaka huu, ilikuwa isikilize maombi ya uhalali wa polisi kuendelea
kuwashikilia Manji na wenzake.
“Lakini
kwa kuonyesha nia ovu upande wa jamhuri umeandaa mashitaka ambayo hayaakisi
mazingira ya kesi hiyo,” alidai.
HAKIMU:
SINA MAMLAKA
Baada
ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili, akiwa hospitalini hapo, hakimu
Shaidi alitoa uamuzi na kusema ameona masuala hayo yanapaswa kuongelewa katika
mahakama yenye mamlaka.
Hakimu
Shaidi alisema kwa kuwa DPP hajaipa Mahakama ya Kisutu, mamlaka ya kusikiliza
shauri hilo, hivyo hawezi kuzungumza lolote. Shauri hilo liliahirishwa hadi
Julai 17, mwaka huu kwa kutajwa kwa kuwa upelelezi haujakamilika.
Baada
ya kuahirishwa kwa kesi hiyo saa 10.38 jioni, washitakiwa Kisinda, Sangey na
Fwele waliondolewa hospitalini hapo kwa kutumia gari la polisi aina ya Land
Cruiser, lenye namba T 968 DHS na kupelekwa mahabusu kwenye gereza la Keko,
huku Manji akiwa hospitalini hapo atakuwa chini ya ulinzi wa Magereza.
YALIYOJIRI
KABLA NA BAADA YA KUSOMEWA MASHITAKA
Mapema,
jana mawakili wa washitakiwa hao walifika katika Mahakama ya Kisutu, wakifuatilia
kesi dhidi ya wateja wao.
Ilipofika
saa 8.30 mchana, mawakili wa pande zote wa serikali na utetezi, waliingia
katika chumba cha hakimu Shaidi, ambapo baada ya muda mfupi walitoka na kueleza
kuwa mahakama inahamia Muhimbili kuwasomea mashitaka yao.
Kutokana
na hilo, watu waliokuwepo mahakamani hapo wakifuatilia kesi hiyo, wakiwemo
wafanyakazi wengine wa Manji, waliingia kwenye magari na kwenda Muhimbili,
ambapo mawakili wake waliamua kukodi teksi tatu.
Katika
jengo hilo, kulikuwa na ulinzi mkali wa askari waliovalia kiraia na wale wenye
sare za kazi, ambapo waandishi wa habari waliruhusiwa kutuma wawakilishi wawili,
huku ndugu na jamaa wakizuiliwa kwa kuwa wagonjwa hawahitaji msongamano.
No comments:
Post a Comment