Monday, 10 July 2017

MKAPA AFUNGUKA




RAIS mstaafu Benjamini Mkapa, amewataka Watanzania kubadili fikra na mtazamo kwa kubuni miradi itakayosaidia jamii na taifa kujitegemea ili kuondokana na utegemezi wa mataifa tajiri.

Amesema iwapo wananchi wataendelea na dhana potofu ya kutarajia mataifa makubwa yaje kuinua taifa letu kiuchumi bila juhudi za wananchi, maendeleo ya Tanzania yatazidi kurudi nyuma.

Rais Mkapa aliyasema hayo jana, wakati akifungua jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Kata ya Nkoma wilayani Itilima mkoani Simiyu, ambacho kimejengwa na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Japan kwa thamani ya sh. milioni 270.

Kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia wagonjwa wakiwemo kinamama wajawazito, kupata huduma ya upasuaji karibu, tofauti na awali ambapo walikuwa wakitembea umbali wa kilomita 40 kufuata huduma hiyo.

Rais huyo mstaafu alieleza kuwa, kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha taifa linajitegemea na kuwaletea wananchi wote maendeleo, huku akiwataka wasomi na wafanyakazi kuendesha midahalo na makongamano yenye tija, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha nchi ijitegemee.

“Kila siku utasikia watu wanadai haki, makongamano, midahalo ya kudai haki, swali la kuwauliza je, wao wametimiza wajibu kama Watanzania? Maana hakuna haki bila wajibu. Tubadili fikra na mitazamo na kuendesha makongamano ya kuonyesha nchi itajitegemea vipi,” alisema Mkapa.

Alisisitiza kuwa ili nchi iweze kujitegemea, ni lazima kila Mtanzania akatimiza wajibu wa kufanyakazi kama Rais Dk. John Magufuli, anavyosema na kutolea mfano wananchi wa Japan wanavyojituma kwa kila mmoja kufanyakazi na kwamba, Watanzania pia wanaweza iwapo watakubali kubadilika.

“Kama tunatarajia mataifa yaje kutuinua wakati sisi tumekaa, hiyo ni dhana potofu, viongozi tushirikiane na wananchi kubuni miradi ili tujiendeleze na kujiletea maendeleo sisi wenyewe, kama Japan wanavyofanya,” aliasa Rais mstaafu Mkapa.

Alisema tangu utawala wa Baba wa Taifa na sera za Chama Cha Mapinduzi (CCM), ilikuwa ni ujamaa na kujitegemea, jambo ambalo bado linapaswa kutekelezwa na kila mmoja kwa nafasi aliyonayo kama wajibu.

Rais mstaafu Mkapa aliishukuru Japan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo kupitia taasisi yake, ambayo lengo lake ni kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga.

“Nchi yetu bado tunakabiliwa na changamoto ya vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga. Japan imetoa msaada huu kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya kituo cha afya. Taasisi ya Mkapa Foundation itaendeleza ushirikiano na serikali katika kutatua changamoto za afya,” alisema.

Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga, alisema pamoja na kukamilika kwa jengo hilo, bado kuna upungufu wa watumishi wa afya, hivyo kuiomba serikali iajiri watumishi wa kutosha ili wananchi wapate huduma bora na kwa wakati.

Silanga alisema jengo limeongeza faraja kwa kinamama wajawazito kwani baadhi yao walikuwa wakifia njiani wakati wakisafirishwa kwenda mjini (umbali wa kilomita 40) Bariadi kupata huduma ya upasuji.

Katika hatua nyingine, Mkapa amewasili wilayani Chato mkoani Geita, ambapo leo, anatarajiwa kukabidhi nyumba 10, kwa hospitali ya wilaya hiyo zilizojengwa kwa ufadhili wa Taasisi ya Mkapa.

Mkapa aliwasili jana, wilayani humo, akiwa ameambatana na mkewe Mama Anna.

Kiongozi huyo alipokewa na mwenyeji wake, Rais Dk. Magufuli, aliyekuwa sambamba na mkewe Mama Janeth.

Katika msafara huo, Mkapa aliambatana na Balozi wa Japan nchini, Masaharn Yoshida, ambaye leo, atakabidhi mashine ya kukamulia mafuta ya alizeti kwa Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Chato -AMCOSS.

Pia, Mkapa anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa hadhara leo, utakaohutubiwa na mwenyeji wake, Rais Dk. Magufuli, utakaofanyika katika uwanja wa Mazaina ulioko mjini Chato, saa tatu asubuhi.

No comments:

Post a Comment