Monday, 10 July 2017
VIONGOZI WA DINI WAWATAKA WANASIASA WAACHE KUMSAKAMA RAIS MAGUFULI
MWENYEKITI wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga, amewataka wanaomshambulia Rais Dk. John Magufuli kuacha mara moja.
Badala yake amewataka waelekeze mashambulizi hayo katika kuimarisha kila kijiji, wilaya na mikoa kwa ajili ya kumlinda mtoto wa kike na vitendo vya ubakaji.
Amesema kwa kufanya hivyo, wanafunzi watapata ulinzi wa kudumu kuanzia shule za awali, msingi na sekondari dhidi ya vitendo viovu.
Tamko hilo alilitoa mwishoni mwa wiki, wakati akifunga kongamano la siku mbili, lililowashirikisha vijana 2,783, kutoka Tanzania Bara, ambao ni wajumbe wa kueneza maadili na amani vijijini, kupitia mpango maalumu wa kuwafikia vijana ili kujiepusha na maadili hatarishi ya matumizi ya dawa za kulevya na kupinga elimu ya ugaidi kwa vijana wote nchini.
Askofu Mwamalanga, ambaye amekuwa kwenye mtandao wa kusaidia vijana nchini kwa miaka 16, aliitaja kauli ya Rais Dk. Magufuli kuwa ni ya ukombozi kwa watoto wa kike na wazazi, kwani hakuna mzazi anayempeleka mtoto shuleni kupata mimba.
“Kumshutumu Rais Magufuli ni kitendo cha kulea majambazi wa ubakaji na ndoa za utotoni. Hapa ni lazima serikali iweke ulinzi kwa wanafunzi wa kike wanaosoma shule za mbali na makazi, ikiwa ni pamoja na kuwapima wasichana wote wakati shule zinaanza kwa kila muhula wa masomo," alisema.
Alisema Rais Magufuli kwa hili yupo sahihi kwa asilimia 100, kwani dawa ya dhambi ni kuikataa kwa macho meupe na siyo vinginevyo.
"Kuanzisha mijadala kwamba anawachukia wanawake, siyo sahihi, Rais Magufuli ana mke, watoto kama tulivyo sote, huyu ni mzazi tena Rais wa nchi anayejua tabu na shida pale mtoto wa kike anapobeba mimba na kukatizwa elimu.
"Kauli yake ina maana kwa wanafunzi kuzingatia elimu badala ya mapenzi, kwa watoto wa kike kuishikilia fursa ya elimu bure kwa nguvu kubwa na wenye kusimamia ulinzi kwao kuongeza mkakati huo zaidi na si vinginevyo," alisema.
Pia, aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na miji, kuisimamia kauli ya Rais Dk. Magufuli kwa vitendo kwa kuainisha maeneo hatarishi kwa wanafunzi wa kike ili wawe na ulinzi.
"Vijana hawa kutoka mikoa yote wamekiri kuwa ubakaji ni janga la kitaifa kwa mikoa yote nchini, jambo ambalo limefanya tatizo hilo kuzoeleka na baadhi ya wanafunzi wasiopenda elimu kama njia ya kukwepa masomo ili waolewe," alisema.
Vilevile, aliwaonya baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kuacha mchezo wa kuchezea maisha ya wanawake, badala yake wawe na msimamo chanya wa kumsaidia mtoto wa kike.
"Kuna wanasiasa siku za karibuni walikuwa wakitetea wanafunzi wa kike wakijifungua wawe wanarudi shuleni, siku hizi wamegeuka na wanatetea marufuku ya mtoto huyo huyo kutorudi shuleni, watu wa namna hii hawafai kumsaidia msichana wa kizazi cha leo," alisema.
Aliongeza kuwa, baadhi ya vijana hao, ambao ni walimu wa shule za msingi, wamesema ili kumaliza tatizo la mimba shuleni, ni lazima katazo la Rais lisimamiwe na Wizara ya Elimu, halmashauri za wilaya, madiwani na wenyeviti wa vijiji kwa kuwashirikisha walimu na wazazi.
Kwa upande wake, Shekhe Kassim Rajabu, aliwahimiza vijana hao kwenda kuyatendea kazi yote waliyojifunza kwenye kongamano hilo la aina yake, ambalo limewashirikisha vijana wa dini mbalimbali nchini.
“Twendeni tukawe wajumbe mkoani mwetu ili kuibadilisha jamii ya vijana kutoka kwenye uhalifu mbalimbali, ukiwemo ugaidi, ambao unawanyemelea sana na kuashiria uvunjifu wa amani," alisema Shekhe Rajabu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment