Thursday, 6 July 2017
MAJERUHI ATOLEWA JICHO, IGP ASEMA KITAELEWEKA
MWENYEKITI wa Kitongoji cha Londo, wilayani Kibiti, mkoani Pwani, Michael Martin (28) yuko hatarini kutoona tena baada ya kutolewa jicho la kulia.
Akizungumza na gazeti hili , Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Neema Mwangomo, alisema mwenyekiti huyo mwishoni mwa wiki iliyopita alifanyiwa upasuaji kwa saa mbili na kutolewa jicho la kulia.
Neema alisema baada ya upasuaji huo, jicho la upande wa kushoto lilionekana mishipa yake kupata majeraha makubwa , hivyo alipewa dawa.
Alisema kwa sasa hali yake inaendelea kuimarika baada kufanyiwa upasuaji huo, ambapo jicho lake liliharibiwa na risasi.
Martin alifikishwa Muhimbili Juni 28, mwaka huu, usiku akitokea Hospitali ya Misheni ya Mchukwi iliyopo Kibiti.
Baada ya kufikishwa hospitalini hapo, alipelekwa Idara ya magonjwa ya dharura na ajali, ambapo timu ya madaktari ilimfanyia uchunguzi na kugundua jicho lake la kulia limepasuka.
Pia, Neema alisema uchunguzi huo ulibaini jicho la kushoto mishipa ya fahamu imejeruhiwa na kumfanyia upasuaji, Juni 29, mwaka huu.
Mwenyekiti huyo alijeruhiwa katika mauaji yaliyotokea Kibiti ambayo yalimpoteza Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mangwi, Mwarami Shamte na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Hamis Mtima.
Wakatio huo huo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Simon Sirro amesema suala la Kibiti linaenda vizuri na kuonya kuwa kama kuna watu wametumwa kwa ajili ya kuvuruga amani ya Tanzania, watapata majibu yao.
"Wale ambao wametumwa vibaya, nasi tutawajibu vibaya, hivyo wasubiri majibu yao. Sisi Watanzania hatujazoea vurugu kama hizo kwa sababu ni wamoja na tunapendana," alisema Sirro.
Aliwaomba Watanzania kuwa na ulinzi wa umma, shirikishi kwa ajili ya kujilinda na uhalifu.
"Naowaomba wananchi wa Kibiti na Ikwiriri kuanzisha ulinzi shirikishi ili waweze kujilinda...kwa sababu kuna maeneo mengine ya ndani ndani pikipiki za polisi zinashindwa kufika,"alisema Sirro.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limekabidhiwa magari manne aina ya Haval Suv na Kampuni ya Great Wall ya nchini China.
Magari hayo yalikabidhiwa jana kwa Sirro katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi lililopo Oysterbay, Dar es Salaam.
IGP Sirro aliishukuru kampuni hiyo na kuahidi kuhakikisha magari hayo yanawasaidia Watanzania ili kutatua changamoto za uhalifu.
Naye, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Great Wall, Jianguo Liu, alisema wamekabidhi magari hayo ili yaweze kusaidia jeshi hilo katika kazi zake za kulinda usalama wa Watanzania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment