Thursday 31 August 2017

MANGULA AWATAKA MABALOZI WA MASHINA KUJIPANGA




MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara) Phillip Mangula, amewataka mabalozi wa mashina kujipanga na kuhakikisha wanashinda kwenye uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020.

Pia, amewataka watendaji hao kuwa madaktari kwenye mashina, kata, mitaa na wilaya zao kwa kutumbua majipu ya mafisadi wa mali za Chama.

Kauli hiyo aliitoa jana, kwenye semina elekezi ya mabalozi na makatibu wa mashina wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam.

Alisema mabalozi ni jeshi kubwa, hivyo wanatakiwa kujipanga na kuhakikisha majimbo na serikali za mitaa zilizochukuliwa na upinzani, zinarudi CCM.

"Mjipange upya ili kuhakikisha uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020, tunafanya vizuri. Pia, ongezeni wanachama kwenye mashina yenu ili CCM iwe na wanachama wengi,"alisema.

Akizungumzia uchaguzi ndani ya Chama, aliwataka kuwachagua watu ambao watakuwa waaminifu ndani ya CCM na ambao hawataishi nao kwa mashaka.

"Mwanachama au kiongozi ni lazima awe mwaminifu, msije mkafanyakosa la kumchagua mtu ambaye mtaishi naye kwa mashaka," alisema.

Kuhusu kutumbua majipu, alisema viongozi wa CCM kuanzia ngazi za chini, watakiwa kutumbua majipu kama anavyofanya Rais Dk. John Magufuli ili kukipa heshima Chama.

Vilevile, aliwataka viongozi hao kulinda mali za Chama na ikiwezekana watoe taarifa kwenye kamati za siasa, inapotokea kuna ubadhilifu au upotevu wa mali za chama.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alisema watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa uaminifu.

"Wale waliotaka kudandia dandia, salamu naona wanazipata. Tutaitekeleza Ilani kwa uaminifu mwingi na kuhakikisha inatekelezeka,"alisema.

Pia, aliwaomba viongozi wa CCM waliochaguliwa, wawe waadilifu na watoe huduma kwa wananchi wao ili waweze kukipenda Chama.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu CCM Wilaya ya Ubungo, Salum Kali, alisema chama wilayani kina changamoto, ikiwemo kukosekana kwa ofisi kutokana na wilaya hiyo kuwa mpya.

Alisema wilaya hiyo ina kata 14, matawi 137, majimbo mawili na wanachama wa 76,850.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Saad Kusilawe, alisema baada ya kukamilika kwa uchaguzi wa CCM katika wilaya hiyo, wanatarajia kufanya ziara kwa ajili ya kutembelea mashina ili kujua utendaji kazi wao.

No comments:

Post a Comment