Thursday 31 August 2017

RC MAKALLA ASIMAMISHA LIKIZO ZA WAKUU WA WILAYA NA WAKURUGENZI


MKUU wa Mkoa Mbeya, Amos Makalla, amesema amesimamisha likizo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wote, hadi pale atakapokamilisha kazi ya kuchagua aina ya mazao wanayotaka  kuyaongezea thamani.

Amesema hakuna haja ya wilaya kuwa na viwanda vikubwa, bali kuhakikisha kunakuwepo viwanda vidogo, vitakavyokuwa na jukumu la kuongeza thamani ya aina ya mazao yatakayoteuliwa kwa kila wilaya.

Makalla aliyasema hayo jana, wakati akizungumza na madiwani kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Chunya, lililokutana kujadili taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Alisema kuna baadhi ya watu wanafikiri kuwa serikali kuu iliposema kuhusu viwanda, itapeleka fedha kwenye wilaya kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vikubwa, jambo ambalo siyo sahihi kabisa.

“Tunatakiwa kuwa na viwanda vidogo, mfano viwanda vya kuongeza thamani ya zao la asali, ambalo lina soko kubwa duniani. Mfano, mnaweza mkawekeza nguvu katika kuongeza thamani ya zao la alizeti, kwa kuhakikisha wananchi wanahamasishwa kulima kwa wingi,” alisema Makalla.

Aliongeza kuwa wilaya ya Chunya inao uwezo wa kulima zao la alizeti, kwani hali ya hewa inawaruhusu, hivyo kinachotakiwa ni kuwahamasisha zaidi wananchi ili walime zao hilo.

Alisema binafsi yuko tayari na amemshawishi mwekezaji mmoja, kwenda wilayani humo kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti.

Mkuu huyo wa mkoa alisema ili kuhakikisha kila halmashauri inateua zao moja ama zaidi kwa ajili ya kuyaongezea thamani, amesimamisha likizo kwa wakuu wote wa wilaya na wakurugenzi watendaji wao hadi wahakikishe wameikamilisha kazi hiyo.

Katika hatua nyingine, Makalla alisema Halmashauri ya Chunya ina matatizo makubwa katika suala la utunzaji  wa mazingira, hatua iliyosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

“Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia hii kama kete yao ya kisiasa.
Chunya imevamiwa sana katika mapori na hifadhi za misitu zilizotengwa kwa mujibu wa sheria, lakini taratibu zimekuwa zinakiukwa makusudi na tumekuwa wavumilivu,” alisema Makalla.

Aliongeza kuwa uongozi wa serikali mkoa, umeona utumie busara zaidi ili kuwapa muda wale wote waliovamia mapori na hifadhi za misitu, waondoke wenyewe kwani ifikapo Septemba, mwaka huu, operesheni kubwa ya kuwaondoa kinguvu itafanyika.

Makalla aliwaeleza madiwani kuwa, huu ndiyo msimamo wa serikali kwamba, msimu huu yeyote aliyevamia pori ama hifadhi ya msitu, ni vyema aondoke mwenyewe na ndiyo maana ametoa taarifa mapema.

"Waanze kuhama wenyewe pole pole, hivyo madiwani nendeni mkawaambie wasianze kulima tena msimu huu kwenye mapori ama hifadhi za misitu walizovamia, kwani wasipotekeleza  hili ni wazi watakuwa wakorofi,” alisema.

No comments:

Post a Comment