Thursday 3 August 2017

RC GAMBO: TUNASHANGAZWA BIDHAA ZA TANZANIA KUZUIWA KUINGIA KENYA

Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe Gambo akipokea maelezo toka kwa Afisa wa forodha mpakani Namanga bwana Mohamed Tukwa (wa kwanza kushoto) wakati akizungumza na madereva wa malori waliokwama mpakani hapo.

Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe Mrisho Gambo ametembelea mpaka wa Namanga na kusikitishwa na kitendo cha malori zaidi ya 40 yaliyobeba unga wa ngano ya wafanyabiashara toka Tanzania yaliyokua yakielekea nchini Kenya kuzuiliwa kuingia nchini humo kwa takribani siku nane sasa licha ya changamoto zilizokuwepo baina ya nchi hizo kutatuliwa.
Gambo ameshangazwa na kitendo cha nchi ya Kenya kuendelea kuzuia bidhaa toka Tanzania ilhali bidhaa toka Kenya kuruhusiwa kupita katika mpaka huo hali ambayo amesema imewasababishia hasara kubwa wafanyabiashara wa Tanzania.
“Hapo.
 katikati kumekua na changamoto lakini pande mbili zilishakaa na kwa upande wa Tanzania vizuizi vyote vilishaondolewa, bidhaa zinazotoka Kenya kuja kwetu wanazi”clear” zinaendelea sasa tunashangaa kuona kwanini bidhaa za kwetu zinazuiliwa kwenda upande wa Kenya na hasa ukizingatia masharti yote ya msingi ya biashara mmeshayafuata” Gambo aliwaeleza madereva wa Tanzani waliokwama katika mpaka huo upande wa Kenya.
Awali Kaimu Afisa forodha wa mpaka huo upande wa Tanzania Mohamed Tukwa amesema licha ya kufanya jitihada mbalimbali za kuwasiliana na wenzao wa upande wa Kenya bado hakuna suluhu ya kuruhusu bidhaa zetu kuingia kwao.
“Na baada ya kufuatilia leo asubuhi alikuja afisa wa forodha toka Kenya kuja kueleza ni nini kinaendelea upande wa Kenya na wanasema mpaka sasa hawajapata maelekezo yoyote toka kwa viongozi wao wa juu kuruhusu malori toka Tanzania kuingiza unga wa ngano na gas ya LPG toka Tanzania” alisema bwana Tukwa.
Nao baadhi ya madereva wa malori wanaolekea nchini Kenya wamedai kuwa hadi hivi sasa hawajui kinachoendelea kwani wapo hapo kwa takribani siku nane hali ambayo wanadai imewasababishia usumbufu mkubwa.
Viongozi mkoani Arusha wapo katika harakati za kutafuta suluhu ya mkanganyiko huo kwa kushirikisha viongozi wa juu wa serikali kwakua jambo hili lina sura ya kidiplomasia.

No comments:

Post a Comment