Thursday 7 September 2017

WABUNGE WATOA YA MOYONI WIZI WA MADINI YA TANZANITE



BAADHI ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamesema chanzo kikubwa cha serikali kuibiwa mabilioni ya fedha katika sekta ya madini, ni ubinafsi wa watendaji wake na kuweka mbele zaidi maslahi yao binafsi.

Wamesema wamechoka kuiona nchi ikiibiwa mabilioni ya fedha na wawekezaji, ambao wamekuwa wakishirikiana na maofisa wa serikali, hivyo wakati sasa umefika kwa wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha, wabunge hao wamesema wakati umefika kwa sheria zinazohusu madini na kodi kufanyiwa marekebisho makubwa ili kulinda rasilimali za nchi.

Walitoa kauli hizo juzi, baada ya kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuwasilisha ripoti zake kuhusu mwenendo wa biashara ya madini ya tanzanite na almasi nchini.

Ripoti hizo ziliwasilishwa kwa Spika Ndugai, kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma, ambapo naye aliikabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kabla ya kukabidhiwa kwa Rais Dk. John Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam, jana.

Mbunge wa Chwaka -CCM), Bhagwaji Maganlal Meisuria, alisema siku zote nchi imekuwa ikiibiwa mabilioni ya fedha katika biashara ya madini, hivyo wakati umefika kwa wizi huo kukomeshwa na wahusika kuchukuliwa hatua.

Alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kulinda rasilimali za nchi na kuongeza kuwa, Watanzania wanapaswa kumuunga mkono kwa nguvu zote badala ya kumkatisha tamaa.

Hussein Bashe (Nzega-CCM), alisema wizi unaofanywa na wawekezaji katika biashara ya madini, wakisaidiwa na maofisa wa serikali, unafahamika vyema na viongozi wa nchi, hivyo unapaswa kukomeshwa.

Alisema haiingii akilini kuona waziri mwenye dhamana ya madini, anaingia mikataba ama kuruhusu mambo mazito yafanyike bila kupata baraka za viongozi wakuu wa nchi.

“Wametajwa viongozi wengi, wakiwemo waliowahi kuwa mawaziri wa wizara ya nishati na madini, mimi naamini yaliyofanyika viongozi wa juu wana msukumo ndani yake,”alisema mbunge huyo.

Bashe alisema uwekezaji katika madini umesababisha madhara makubwa katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo uharibifu wa mazingira huku ukiwa hauna manufaa kwa Watanzania.

"Nawapongeza sana wabunge wa kamati, wametumia muda mfupi, lakini wamekuja na ripoti ambayo imetoa picha halisi ya uwekezaji wa madini nchini,”alisema.

Felister Bura (Viti Maalumu-CCM), alisema wanapongeza hatua iliyochukuliwa na bunge ya kuunda kamati za kuchunguza biashara ya madini hayo, ambapo zimefanyakazi nzuri kwa muda mfupi.

Upendo Peneza (Viti Maalumu-CHADEMA), alisema kuna umuhimu wa kurekebisha sheria za kodi na zile zinazosimamia rasilimali za nchi ili serikali iweze kunufaika na rasilimali hizo.

Aliishauri serikali kuwa na uwazi katika mifumo ya utendaji ili wasilimbikize makosa kama ilivyo hivi sasa, ambapo watendaji serikalini wamekuwa wabinafsi katika utendaji wao wa kazi na wanajali maslahi yao binafsi.

Raphael Chegeni (Busega-CCM), alishauri serikali kurekebisha sheria zinaweka kinga na kulinda rasilimali za taifa.

Alimpongeza Spika Ndugai kwa uamuzi wake wa kuunda kamati hizo mbili na kuja na majawabu, ambao yamewagusa wananchi wengi.

Aliwataka wahusika wote walioguswa kwenye ripoti za kamati hizo, kujitafakari na ikiwezekana kuachia ngazi ili nchi iendeshwe kwa kufuata sheria.

Magdarena Sakaya (Kaliua-CUF), aliwataka wabunge na Watanzania kuweka kando itikadi za vyama vyao linapokuja suala linalohusu maslahi ya taifa.

Alisema Tanzania ni nchi masikini,  lakini inazo rasilimali nyingi, ambazo iwapo zitatumiwa vizuri, nchi inaweza kunufaika na maisha ya wananchi yakawa bora kuliko ilivyo hivi sasa.

No comments:

Post a Comment