Thursday 7 September 2017

MAJALIWA ATEMA CHECHE WALIOHUSIKA WIZI WA ALMASI NA TANZANITE



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali itayafanyiakazi mapendekezo na ushauri wote uliotolewa na kamati mbili za bunge, zilizoundwa kuchunguza biashara ya madini ya tanzanite na almasi.

Amesema anatarajia kuzikabidhi ripoti hizo leo, saa 4.30 asubuhi kwa Rais Dk. John Magufuli, Ikulu, Dar es Salaam, ili ziweze kufanyiwa kazi mara moja.

Majaliwa alisema hayo jana, baada ya kukabidhiwa ripoti ya kamati hizo na Spika wa Bunge, Job Ndugai, katika hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya bunge, mjini hapa.

"Nimefarijika sana kwa uamuzi wa bunge na serikali itayafanyiakazi mapendekezo yote ya kamati, haitafanya mchezo hata kidogo, lazima viongozi wahakikishe wanatimiza majukumu yao,"alisema.

Alisema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli, imechoshwa na vitendo vya wizi, rushwa, uzembe na ubabdhirifu hivyo huu siyo wakati wa kucheza, lazima ichukue hatua.

Majaliwa alisema anaheshimu utawala wa sheria, vinginevyo angechukua uamuzi papo hapo, lakini lazima akabidhi ripoti hizo kwa Rais Magufuli kabla ya kuchukua hatua.

Alimuomba Spika Ndugai wafuatane katika safari hiyo ya kwenda kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais Magufuli ili kuwaonyesha Watanzania jinsi serikali ilivyopania kuleta mageuzi nchini katika sekta mbalimbali.

Waziri Mkuu alisema lengo la serikali ni kuona kuwa, rasilimali zote nchini zinakuwa mikononi mwa Watanzania, hivyo haiko tayari kuona zikitumiwa na watu wachache kujinufaisha.

Alimpongeza Spika Ndugai kwa kuunda kamati hizo na pia wajumbe wake, ambao alisema wamedhihirisha wazi kuwa ni vichwa.

Alisema yaliyobainishwa kwenye ripoti hizo, hakuna aliyewahi kuyasikia wala kuyatarajia, hivyo kamati zimefanyakazi nzuri na zinastahili kupongezwa na kwamba, serikali itayafanyiakazi mapendekezo yote.

Majaliwa alisema kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda maliasili ya Tanzania, kuitunza na kushiriki katika mapambano dhidi ya ubadhirifu, wizi na rushwa.

Aidha, alitaka kila Mtanzania ashiriki katika kuhubiri uzalendo, kulinda umoja na kuleta mageuzi katika sekta ya madini.

Alisema kuundwa kwa kamati hizo mbili kumeonyesha wazi jinsi bunge lilivyoingilia kati suala hilo kwa miguu miwili kwa lengo la kuonyesha uozo unaofanyika kwenye migodi ya almasi na tanzanite.

Waziri Mkuu alisema kwa sasa serikali imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutungwa kwa sheria zenye kuleta tija na kumnufaisha mwananchi na kwamba, bunge limepewa mamlaka ya kupitia mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi.

Alisema marekebisho yanayofanyika ni ya  Sheria ya Madini sura ya 23, Sheria ya Petroli sura ya 322 na Kodi ya Mapato sura ya 332.

Aidha, alisema serikali inatarajia kuunda Tume ya Madini hivi karibuni ili madini yaongezewe thamani hapa nchini na uchenjuaji nao ufanyike hapa nchini. Alisema tayari kampuni zaidi ya 10 zimejitokeza kutaka kujenga mitambo ya kuchenjua madini.


No comments:

Post a Comment