Thursday 7 September 2017

RIPOTI KAMATI ZA BUNGE ZAZUA MJADALA MZITO



KAMATI mbili za bunge zilizoundwa kuchunguza biashara ya madini aina ya tanzanites na almasi, zimewasilisha ripoti zake kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai huku zikiitaka serikali iwachukulie hatua mawaziri watatu wa zamani wa Wizara ya Nishati na Madini.

Mawaziri hao wa zamani waliotajwa kwenye ripoti hizo ni William Ngeleja, Sospeter Muhongo na George Simbachawene, ambao wanadaiwa kufanya makosa mbalimbali ya kiutendaji walipokuwa wakiiongoza wizara hiyo na kuisababishia serikali kupata hasara ya mamilioni ya fedha.

Mbali na mawaziri hao wa zamani, kamati hizo pia zimeitaka serikali iwachukulie hatua maofisa wa zamani wa Shirika  la Madini Tanzania (STAMICO), akiwemo Dk. Edwin Ngonyani, ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano, wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo na mkurugenzi wa kitengo cha kuthaminisha madini.

Uwasilishaji wa ripoti za kamati hizo ulifanyika jana, kwenye viwanja vya bunge mjini hapa,
mbele ya Spika Ndugai, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, mawaziri, wabunge,  wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, makatibu wakuu wa wizara, viongozi wa taasisi za umma na wawakilishi wa vyama vya siasa.

Akiwasilisha ripoti ya biashara ya madini ya tanzanite, Mwenyekiti wa kamati hiyo,  Doto Biteko, alisema mwenendo wa baadhi ya viongozi katika usimamizi wa uchimbaji na biashara ya madini hao haukuwa mzuri, hivyo kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha.

Akitoa mfano, alisema Ngeleja anapaswa kuisaidia serikali kutoa maelezo kwa nini aliruhusu STAMICO kuendelea na mkataba na Kampuni  ya TML, licha ya kushauriwa kuwa, mkataba huo haukuwa na tija kwa Tanzania.

Kwa upande wa Muhongo, alisema anapaswa kutoa maelezo kwa nini aliruhusu kutolewa kwa leseni 490 za uchimbaji madini bila kushauriana na Bodi ya Madini wakati Simbachawene anapaswa kueleza kwa nini aliridhia uhamisho wa TML kwenda kampuni mpya ya Sky Associate Limited bila kuzingatia ushauri aliopewa, jambo lililoisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh. bilioni 21.

Biteko alisema mbinu zinazotumiwa na wachimbaji na wauzaji wa madini ya tanzanite zinaikosesha serikali mapato huku biashara hiyo ikigubikwa na wizi, ambapo asilimia 80 ya madini hutoroshwa kwenda katika nchi za India, Kenya, Hong Kong na Marekani na kuifanya serikali iambulie asilimia 20 zinazolipiwa mirahaba.

Alisema serikali imekuwa ikipata hasara kila mwaka kutokana na usimamizi na udhibiti mbovu wa biashara ya madini huku utoaji wa leseni za uchimbaji ukifanyika bila kufuata.

Akitoa mfano, alisema kufuatia marekebisho ya sheria ya madini yaliyofanywa na serikali, leseni za uchimbaji wa madini zinapaswa kumilikiwa na Watanzania  au zimilikiwe kwa kiwango sawa cha asilimia na wawekezaji, lakini baadhi ya kampuni, ikiwemo Tanzanite One, inamiliki kwa asilimia 100.

"Baadhi ya leseni zimekuwa zikitolewa kwa kuchanganya madini tofauti, wawekezaji wamekuwa wakipewa upendeleo kwa wahusika kufumba jicho moja na kwa ujumla, serikali haikujipanga kuingia mkataba wa faida na wawekezaji. STAMICO haikuwa na mipango ya biashara,"alisema.

Alisema STAMICO imekuwa ikipata hasara tangu siku ya kwanza ilipoingia mkataba na TML, lakini iwapo mkataba huo  ungeboreshwa, ingeweza kupata sh. bilioni 19 zikiwa malipo ya mrahaba.

Alisema katika kuingia ubia kati yake na TML, bodi haikuzingatia ushauri wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, ambaye alishauri kuboreshwa kwa maeneo kadhaa yaliyomo kwenye mkataba huo, lakini hayakufanyiwa kazi.

Biteko alisema pia kuwa, TML ilitoa taarifa za uongo kwa STAMICO kuhusu usajili  wake ambapo uchunguzi wa tume umebaini kuwa, haikusajiliwa BRELA.

Kwa mujibu wa Biteko, kamati  yake imefanikiwa kupata mkanda wa wizi wa tanzanite unavyofanyika kwenye mgodi wa Tanzanite One, ukiwahusisha maofisa wa serikali na kwamba, wataukubidhi kwenye mamlaka husika kwa ajili ya wahusika kuchukuliwa hatua.

"STAMICO imekuwa ikisuasua, imeingia kwenye gari lisilo na mwelekeo. Imekuwa ikisuasua katika uteuzi wa wajumbe wa kamati ya uendeshaji. Uteuzi wa wajumbe hauzingatii maelekezo ya wizara ya wahusika wawe wataalamu wa madini,"alisema.

Biteko alisema madini mengi ya Tanzania yamekuwa yakitoroshwa nje ya nchi bila kujulikana thamani yake na kuongeza kuwa, Sky Associate, ambayo iliuziwa hisa na TML, nayo haijasajiliwa BRELA na haina hati ya kufanya biashara nchini.

Kufuatia kuwepo kwa mapungufu hayo, Biteko alisema kamati yake inapendekeza kwa serikali kuzuia utoaji leseni holela za uchimbaji madini, mkataba kati ya STAMICO na TML hauna manufaa, hivyo usimamishwe na kampuni zote za TML zilizo ndani na nje ya nchi ziwekwe chini ya ulinzi.

Mapendekezo mengine ni mwenendo wa baadhi ya viongozi na wataalamu wa serikali sio mzuri, hivyo wachukuliwe hatua na kwamba, serikali ifanye ukaguzi wa leseni 435 zilizotolewa kwa wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati iliyochunguza biashara ya almasi, Mussa Azzan Zungu alisema serikali haijafanya utafiti ili kujua kiwango cha almasi kilichoko katika machimbo ya Mwadui, ndio sababu wawekezaji wamekuwa wakifanya wizi mkubwa wa madini hayo.


Zungu alisema iwapo hali hiyo haitarekebishwa, mgodi wa Williamson ulioko Mwadui, utaacha athari kubwa kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo hayo, yakiwemo ya kiafya.

Alisema kuanzia mwaka 2007 hadi 2017, mgodi wa Williamson haujalipa kodi, inayokadiriwa kufika sh. bilioni moja kwa kisingizio cha kupata hasara na kuhoji kama inapata hasara, kwa nini inaendelea kuwepo kwenye eneo hilo na kutumia fedha nyingi kwenye uwekezaji.

"Kama leseni ya kampuni hii itaendelea kufanyakazi, serikali itaendelea kupata hasara kubwa. Kama wanapata hasara, kwa nini hawaondoki?" Alihoji.

Zungu pia alisema kamati yake imebaini kuwa, ripoti ya Wizara ya Nishati na Madini na ile ya Wakala wa Ukaguzi, kuhusu mauzo ya almasi zimekuwa zikitofautiana na kwamba, hakuna ushirikiano mzuri kati ya wizara na taasisi zake.

Alisema almasi yenye thamani kubwa duniani inapatikana Tanzania, lakini Botswana imekuwa ikiuza kwa bei kubwa kuliko Tanzania.

Aidha, alisema kitendo cha madini ya almasi kuuzwa nje bila kuthaminiwa na kusafishwa hapa nchini, kimekuwa kikiikosesha serikali mapato mengi na kwamba, hilo lilianza kufanyika baada ya Kampuni ya Tancut ya Iringa kusimamisha shughuli zake.

Zungu alisema usimamizi mbovu wa serikali katika mgodi wa almasi wa Williamson huku wakiwa hawana nyenzo muhimu, nao umekuwa ukichangia kuwepo kwa wizi mkubwa wa madini hayo unaofanywa na wawekezaji na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Alisema mwakilishi wa serikali katika mgodi huo,anao ufunguo wa eneo la x-ray, lakini hana ufunguo wa eneo lingine muhimu huku kukiwa na mlango wa dharula katika eneo hilo, ambao hutumiwa na wamiliki wa mgodi huo kutorosha madini.

"Hivi kwa nini usafishaji wa madini haya usifanyike nchini? Watendaji wamekuwa wakitumika kuhujumu mapato ya nchi. Kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa kitaalamu katika uthaminishaji wa madini, ambao hivi sasa wapo wawili tu na wamekuwa wakifanyakazi hiyo kwa miaka 18, kamati haoni sababu kwa nini utaalamu huo wasifundishwe wengine,"alisema Zungu.

Kwa mujibu wa Zungu, gharama za uendeshaji zimekuwa zikibambikwa na kampuni hiyo, ikiwemo mitambo feki, ambayo hununuliwa kwa bei ya chini, lakini imewekwa bei ya mitambo mipya.

Alisema mthaminishaji wa madini ndiye mwamuzi wa mwisho, hakuna wa kumuhoji, hivyo ana uwezo wa kuyathaminisha madini kwa bei ndogo, lakini yanapouzwa nje, bei inakuwa kubwa.

Zungu alisema fedha za mauzo ya almasi zimekuwa zikiwekwa kwenye benki za nje na kampuni husika, hivyo kuifanya serikali kutofaidika na fedha hizo, badala yake kampuni husika ndizo zinazofaidika zaidi.

Aliutaja udhaifu mwingine uliobainika katika uchunguzi wa kamati yake kuwa ni mikopo ya wawekezaji kutohakikiwa na benki, kampuni zinapofunga biashara kwa kisingizio cha kupata hasara, zinahamishia umiliki kwa kampuni zingine zenye uhusiano na kwamba, migodi ya madini nchini imewekwa rehani kutokana na madeni makubwa.

Kufuatia kubainika kwa kasoro hizo, kamati hiyo imependekeza ufanyika uhakiki wa gharama za uwekezaji kuanzia mwaka 1994 hadi sasa, wajumbe wa bodi wawajibishwe, ufanyike uchunguzi wa mitambo ya mgodi, waliohusika na mikataba mobovu wachukuliwe hatua.

Baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hizo, zilikabidhiwa kwa Spika Ndugai, ambaye naye alizikabidhi kwa Waziri Mkuu Majaliwa, ambaye aliahidi kuzikabidhi kwa Rais Dk. John Magufuli leo, saa 4.30, Ikulu, Dar es Salaam.

Spika Ndugai aliunda kamati hizo kupitia Waraka wa Spika namba 3 wa mwaka huu.
Hadidu za rejea za kamati hizo ni kuchambua taarifa za tume na kamati mbalimbali zilizowahi kuundwa na serikali kwa ajili ya kushughulikia mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya almasi na tanzanite nchini na kutoa mapendekezo yake na namna yalivyotekelezwa na serikali.

Nyingine ni kutathmini mfumo uliopo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa biashara ya madini hayo na kubainisha manufaa, ambayo serikali inapata kutokana na uwekezaji uliopo katika madini hayo na kubainisha na kushauri kuhusu utaratibu bora unaoweza kutumika katika kusimamia uwekezaji, uchimbaji na biashara ya madini ya almasi nchini.

Hadidu nyingine ni kushughulikia jambo jingine lolote linalohusiana na mfumo wa uchimbaji, usimamizi na udhibiti wa madini hayo nchini.

Wajumbe waliounda kamati ya almasi, mbali na Mwenyekiti wake, Zungu ni Dk. Immaculate Sware (Viti Maalumu-CHADEMA), Shally Raymond (Viti Maalumu-CCM), Rashid Ali Abdallah (Tumbe-CUF), Allan Kiula (Iramba Mashariki-CCM), Restituta Mbogo (Viti Maalumu-CCM), Ahmed Juma Ngwali (Wawi -CUF). Wengine ni Richard Ndassa (Sumve-CCM) na Emmanuel Mwakasaka (Tabora Mjini-CCM).

Wajumbe waliounda kamati  ya tanzanite ni Mwenyekiti, Dotto Biteko (Bukombe-CCM),
Mohamed Mchengerwa (Rufiji-CCM), Ezekiel Maige(Msalala-CCM), Balozi Adadi Rajab(Muheza-CCM), Dk.Mary Mwanjelwa(Viti Maalum-CCM), Subira Mgalu (Viti Maalumu-CCM), Juma Hamad Omary (Ole-CUF), Latifa Chande (Viti Maalumu-CHADEMA),  James Ole Millya (Simanjiro-CHADEMA).

No comments:

Post a Comment