Thursday 7 September 2017

SPIKA NDUGAI ASHAURI WIZARA YA NISHATI NA MADINI ITENGANISHWE


SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, ameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuitenganisha Wizara ya Nishati na Madini, ili iweze kufanyakazi zake kwa umakini na kupunguza matatizo, ambayo yamekuwa yakijitokeza katika sekta ya madini.

Ndugai amesema kwa hali ilivyo sasa, wizara hiyo imekuwa ikikabiliwa na mzigo mkubwa wa kusimamia masuala yanayohusu madini na nishati, hivyo kusababisha usimamizi mbovu hasa katika sekta ya madini.

Alitoa ushauri huo jana, baada ya kukabidhiwa ripoti za kamati mbili alizoziunda kwa ajili ya kuchunguza biashara ya madini ya almasi na tanzanite. Hafla hiyo ilifanyika kwenye viwanja vya bunge mjini hapa.

Aliwapongeza wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo kwa kuibua uozo mkubwa ulioko  kwenye uchimbaji na uuzaji wa madini hayo, hali iliyosababisha serikali ikose mapato huku wajanja wachache wakiitumia fursa hiyo kujineemesha.

Ndugai alisema wakati sasa umefika kwa Watanzania kusimama kidete kulinda rasilimali za nchi, badala ya kumwachia Rais Dk. John Magufuli pekee.

"Watanzania sasa tunapaswa tuwe wamoja, tushirikiane. Yako mambo tunapaswa kuwa wamoja. Hata katika familia kuna tofauti, lakini yapo mambo mengine inakuwa pamoja,"alisema Spika Ndugai.

"Kwenye vita, ukimuona mwanakijiji mwenzako anashambuliwa na wanakijiji jirani, unaingilia kati kumuokoa, vivyo hivyo kwa masuala yanayoihusu nchi yetu, tuwe wamoja,"alisisitiza.

Spika Ndugai alisema katika ripoti zote mbili zilizowasilishwa kwake, imedhihirika wazi kuwa,  tatizo la mikataba mibovu kati ya serikali na wawekezaji limekuwa sugu, hivyo wakati umefika kwa suala hilo kusimamiwa kwa umakini.

Alisema inashangaza kuona kuwa, mikataba ya uwekezaji inatayarishwa na wawekezaji kutoka nje na kutiwa saini na maofisa wa serikali huku wahusika wakiwa wamesomea vizuri fani hiyo na kuwa na ujuzi wa kutosha.

"Wasimamizi wengine wakiwemo mawaziri, hawasomi mikataba. Bodi ni chombo muhimu, bila kuwa na bodi hakuna kitu. Tuache kuteua wajumbe wa bodi kwa kujuana.

"Ipo siku mawaziri tutawaita hapa ili mtueleze mliwateua wajumbe wa bodi kwa kutumia kigezo gani. Tukifanya hivyo nawaambia mtatoka mate,"alisisitiza Spika Ndugai.

Alisema katika kuunda bodi, jambo la muhimu kuzingatiwa sio uprofesa au udaktari, ni zaidi ya hapo, ambapo alitoa mfano wa kamati alizounda kuchunguza biashara za madini hayo kwamba, zinaundwa na watu wa kawaida, lakini makini katika utendaji wa kazi.

"Mimi nimeweka  watu wa kawaida, lakini si mmeona matokeo? Hii ni kazi ngumu, walioguswa msikasirike. Baadhi ya mambo hayakusemwa, wamewastahi wahusika. Pengine ndani ya ripoti kuna makubwa zaidi,"alisisitiza.

Alisema inashangaza kuona kuwa, mzigo wa madini unasafirishwa kutoka mgodini ukiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa Tanzania, wakiwa na bunduki hadi Dar es Salaam, na  kusafirishwa kwenda nje huku serikali ikiwa inaibiwa bila kujitambua.

Alisema katika hali ya sasa, ambapo wananchi wanakabiliwa na matatizo ya huduma za afya, maji na chakula, haipendezi kuona rasilimali za Tanzania zinatumika vibaya badala ya kuwanufaisha wananchi.

Alisema baadhi ya wapigania uhuru kutoka nchi za kusini mwa Afrika, zilizosaidiwa kupigania uhuru na Tanzania, wanapotembelea nchini, hushangaa kuona hakuna maendeleo yoyote.

"STAMICO imetuangusha sana, kama mtakumbuka vizuri waheshimiwa wabunge mlimfukuza meneja wa STAMICO alipokuja bungeni, hivi hii STAMICO ni kitu gani," alihoji Spika Ndugai.

Awali, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alimpongeza Spika Ndugai kwa kuunda kamati hiyo bila kujadili tofauti ya itikadi za vyama vya siasa na kuongeza kuwa, kazi zilizofanywa na kamati hizo ni za kihistoria.

Alisema uamuzi huo wa Spika Ndugai umelipa meno bunge na kwamba, linapoamua kufanyakazi kwa kufuata katiba, litakuwa na msaada mkubwa kwa serikali.

Mbowe alisema bunge limejaa watu wenye uzoefu na ujuzi wa mambo mbalimbali, hivyo likitumika vizuri, linaweza kufanya mambo makubwa zaidi.


Hata hivyo, alitaka haki itendeke kwa wote walioguswa kwenye ripoti za kamati hizo na kusisitiza kuwa, serikali isipatwe na kigugumizi katika kuchukua hatua, bila kumuonea mtu, lakini pia haki isipindishwe katika kuwashughulikia wahusika.

Alisema ushirikiano ulioonyeshwa na wajumbe wa kamati hizo katika kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa, usiishie hapo, bali uendelee katika mambo mengine muhimu yanayowahusu Watanzania.

No comments:

Post a Comment