Thursday 7 September 2017

MATANGAZO DAWA ZA NGUVU ZA KIUME MARUFUKU


WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imepiga marufuku matangazo ya biashara yanayohusu dawa za kuongeza nguvu za kiume, iwapo hazijasaliwa na Baraza la Tiba za Asili.

Imesema kuuzwa kwa dawa hizo bila kusajiliwa ni kinyume cha sheria, hivyo lazima wahusika wachukuliwe hatua.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alipokuwa akijibu swali  la nyongeza la Khatib Saidi Haji (Konde-CUF), aliyelalamikia utitiri wa mtangazo yanayohusu dawa hizo kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Waziri Ummy alisema kwa sasa ipo sheria inayohusu tiba asili na tiba mbadala, hivyo dawa zote zinapaswa kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Mbadala kabla ya kutangazwa na kuuzwa mitaani.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Khamisi Kigwangwala, alisema serikali inatambua uwepo wa tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume, japokuwa hakuna jibu la moja kwa moja la kuufahamisha umma kuhusu ukubwa wake kwa kuwa tendo la ndoa ni siri kati ya wanandoa.

Hata hivyo, alisema mwanaume hupungukiwa na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya.

Alisema tatizo hilo kwa kawaida huwapata watu wenye umri mkubwa, kuanzia miaka 60 na wagonjwa wenye magonjwa sugu kama shinikizo la damu, kisukari, kifua kikuu, kansa, ukimwi na wale wanaotumia dawa kwa muda mrefu.

Alisema mwenendo wa wa tatizo hilo kwa sasa umekuwa hauzingatii umri mkubwa, linawapata watu wa rika zote, wakiwemo vijana na watu wazima.

Alisema kwa wazee, tatizo la kupungua nguvu za kiume ni la kawaida na kwamba, wanaume kadri umri unavyozidi kuongezeka, uwezo wa kufanya tendo la ndoa unapungua taratibu na huchangiwa na ukosefu wa afya njema.

No comments:

Post a Comment