Thursday 4 August 2016

KITILYA, WENZAKE WAFUNGUA KESI YA KIKATIBA



ALIYEKUWA Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Harry Kitilya na wenzake watatu, wamefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kuhoji kifungu cha sheria ambacho kinazuia dhamana kwa makosa ya kutakatisha fedha.

Mbali na Kitilya, walalamikaji wengine katika kesi hiyo namba 14 ya mwaka huu, ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na mwanasheria wa benki ya Stanbic Tanzania, Sioi Solomon na Gidion Wasongo.

Kitilya na wenzake wamefungua kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).

Kwa mujibu wa hati ya madai, Kitilya na wenzake wanahoji kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ambacho kinazuia dhamana kwa makosa yanayohusiana na kutakatisha fedha.

Walalamikaji hao wanadai kifungu hicho wanachokihoji kinakwenda kinyume na Ibara ya 13(6)(b) ya  Katiba.

Aidha, wanadai kitendo cha kuwafungulia kosa la kutakatisha fedha hakifanyiki kwa nia njema, bali kwa lengo la kuwazuia kupata dhamana.  Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mahakamani hapo, shauri hilo limepangwa kutajwa leo.

Walalamikaji Kitilya, Shose na Sioi wanakabiliwa na kesi ya msingi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakituhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, katika kuiwezesha serikali kupata mkopo kutoka kutoka Benki ya Standard Uingereza, kupitia mshirika wake, benki ya Stanbic Tanzania.

Kitilya, Shose na Sioi walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili Mosi, mwaka huu, wakikabiliwa na mashitaka manane, likiwemo la kutakatisha fedha.

Hata hivyo, mahakama hiyo iliwafutia walalamikaji hao shitaka la kutakatisha fedha kutokana na kukubaliana na hoja zilizowasilishwa na mawakili wao kwamba, lina upungufu wa kisheria.

Baada ya Kitilya na wenzake kufutiwa shitaka hilo, DPP alikata rufani kupinga uamuzi huo Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment