Thursday 4 August 2016

VIGOGO WAWILI CHADEMA MBARONI



WATU wawili akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) mkoa wa Mbeya, Moses Mwaifunga (28), wametiwa mbaroni na polisi kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mtandao.

Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kutoa lugha ya uchochezi na vitisho, wakiwataka vijana wa chama hicho kuchoma moto ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutoitii serikali.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari, alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa ni kiongozi wa CHADEMA Wilaya ya Mbozi, Meshack Mgaya (28) na kwamba walifikishwa mahakamani jana.

Kidavashari alisema watuhumiwa waliwataka vijana na wafuasi wa CHADEMA kuichoma moto ofisi ya CCM ili Rais Dk. John Magufuli aone nchi sio yake, kufuatia kauli yake ya kuelekeza kila kiongozi afanye mikutano katika eneo lake la uchaguzi.

“Watuhumiwa hawa waliahidi kufanya vurugu ili kuhatarisha usalama wa nchi na kuleta uvunjifu wa amani,” alisema Kidavashari.

Aliongeza: “Julai 29, mwaka huu, ujumbe huo ulitumwa na kusambazwa kwenye makundi ya kijamii, ambapo baada ya polisi kuuona ujumbe huo, waliufuatilia ili kubaini watu waliohusika kuuandaa na kuusambaza ujumbe huo wa uchochezi.”

Kidavashari alisema Julai 31, mwaka huu, saa 12:00 jioni, polisi walimkamata Mwaifunga na baada ya kufanyiwa upekuzi, alikutwa na simu ambazo zilitumika kusambaza ujumbe huo.

“Katika kumhoji, ilibainika Mwaifunga, ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa BAVICHA mkoa Mbeya na kupitia kwake, tulifanikiwa kumpata mtuhumiwa mwingine Mgaya, ambaye ni kiongozi wa CHADEMA wilaya ya Mbozi,” alisema.

Alisema polisi inaendelea kuwatafuta watu wengine wawili, ambao walishiriki kuandaa na kuusambaza ujumbe huo, aliowataja kuwa ni Emma Kimambo na Morris Chonanga, ambaye ni kiongozi wa chama hicho wilaya ya Chunya.

Kidavashari alisema vijana wengine walioshiriki kusambaza ujumbe huo wanaendelea kusakwa na kwamba, wamesambaa katika mikoa ya Morogoro, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Geita.

Aliwataka wananchi kuacha kuwa na imani potofu kwa kutaka kuvunja amani ya nchi kwa kisingizio cha kutaka demokrasia kwa madai kuwa hakuna haki bila wajibu.

No comments:

Post a Comment