Saturday, 2 January 2016

DK. SHEIN: MAZUNGUMZO YA AMANI ZANZIBAR YANAENDELEA VIZURI


NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein, amesema mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa Zanzibar kwa njia ya amani, yamefikia hatua kubwa na taarifa kamili itatolewa yatakapokamilika.

“Mazungumzo hayo yanayowahusisha viongozi sita yamefi kia hatua kubwa na bado yanaendelea na taarifa kamili ya mazungumzo hayo itatolewa mara yatakapokamilika,” alisema Dk. Shein.

Alisema hayo jana katika risala yake ya kuuaga mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 aliyoitoa Zanzibar. Dk. Shein alisema mazungumzo hayo yanafuatia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi huo baada ya kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa kama zilivyoelezwa na tume hiyo. ZEC ilitangaza kufuta matokeo ya urais wa Zanzibar na uwakilishi baada ya kubainika kwa kasoro hizo.

Dk. Shein alisema kuwa katika suala zima la hali ya kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa uchaguzi Mkuu, viongozi walishauriana kukutana ili kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu kwa njia ya amani, ili nchi iendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano na hatimae wakakubaliana kuanza mazunguzmo hayo.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi kuwa Januari 12, mwaka huu Zanzibar itaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ambapo kama kawaida, sherehe hizo zitatanguliwa na matukio mbalimbali ya shughuli za uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika matukio mbalimbali yaliyopangwa katika maadhimisho hayo ambapo pia, kushiriki kwao kwenye sherehe ya maadhimisho hayo ni hatua ya kuyaendeleza malengo ya Mapinduzi kwa shabaha ile ile waliokuwa nayo waasisi wa Zanzibar.

Pia, alitoa wito kwa wananchi kuzingatia kanuni za afya kwa kuimarisha usafi na kuyataka Mabaraza ya Manispaa na Miji kwa Pemba na Halmashauri zote za wilaya kuchukua hatua za uzoaji wa taka huku akihimiza wananchi washiriki kusafi sha miji na maeneo wanayoishi. 


Kuhusu uchumi, Dk. Shein alisema takwimu za robo mbili za mwanzo wa mwaka 2015, zinaonyesha uchumi wa Zanzibar umeendelea kuimarika.

Alisema huduma za jamii zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za afya na na elimu nazo zimeimarika ikiwa ni pamoja na kupiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu. 


Dk. Shein alisema ujenzi wa barabara muhimu umemalizika na kuzinduliwa Unguja na Pemba pamoja na kukiimarisha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume na Kiwanja cha Ndege cha Pemba ambacho tayari kimeshatiwa taa za kurukia ndege.

Alisema kuwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa viwanja hivyo tayari imepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya ndege za kimataifa zinazokuja Zanzibar, jambo ambalo limesababisha kuimarika kwa sekta ya utalii na shughuli za biashara. 


Pia, alisema serikali imefanikiwa kutengeneza meli mpya yenye mitambo ya kisasa katika Kampuni ya ëDaewoo Internationalí ya Jamhuri ya Korea ambayo ina utaalamu na uzoefu mkubwa wa kutengeneza meli.

No comments:

Post a Comment