Friday 29 January 2016

MAJALIWA ACHARUKA



SERIKALI imesema Jeshi la Polisi litaendelea kulinda amani na utulivu kwa wananchi wote na litalazimika kutumia nguvu pale linapoona kuna tishio la kutoweka kwa amani. 

Mbali na hilo, imesema chama chochote cha siasa kitaruhusiwa kufanya mikutano yake pale kitakapofuata taratibu na sheria za nchi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema hayo jana, bungeni mjini hapa, alipokuwa akijibu  swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo.

Alisema serikali ya awamu ya tano inaongoza kwa kufuata misingi ya haki na demokrasia na kwamba, inaheshimu utawala wa sheria kwa mujibu wa Katiba. 


Alisema majeshi yaliyopo nchini, likiwemo la Polisi, yapo Tanzania Bara na visiwani kwa ajili ya kuhakikisha amani na utulivu ndani ya nchi vinadumishwa.

Majaliwa alisema majeshi hayo yanaweza kutumia nguvu kama utaratibu haukufuatwa au kuvunjwa kwa taratibu. 


Alisema jambo la muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kuwa Jeshi la Polisi linasaidiwa kwa watu kufuata taratibu ili liweze kufanyakazi yake vizuri bila kulazimika kutumia nguvu.

Akizungumzia masuala ya siasa, Majaliwa alisema siasa haikuanza leo, hivyo kinachotakiwa ni kufuata taratibu pale chama cha siasa kinapotaka kufanya shughuli zake.

Majaliwa alisema iwapo chama kinataka kufanya mkutano ni lazima Jeshi la Polisi lijiridhishe kama hakuna uvunjifu wa amani na taratibu hizo zikifuatwa, kitaruhusiwa kufanya mikutano yake.

Akizungumzia kauli yake aliyoitoa hivi karibuni akiwa jimboni kwake Ruangwa, ya kukataza mikutano katika jimbo hilo, Majaliwa alisema tamko hilo alilitoa kama mbunge na sio kama Waziri Mkuu.


 Alisema baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, madiwani katika jimbo hilo wakiwemo wa upinzani, walikubaliana kuwa masuala ya siasa yameisha hivyo sasa waungane na kufanyakazi.

“Suala hilo tulizungumza wote kwa pamoja kwani baadhi ya kata zinaongozwa na madiwani wa kutoka upinzani, lakini wote kwa pamoja kama madiwani, tulikubaliana kuwa siasa imepita na kilichobaki ni kufanyakazi ili kuleta maendeleo katika jimbo hilo,’’ alisema.

Aliongeza: “Mimi naheshimu utawala wa sheria, hivyo tamko nililitoa kama mbunge wa Ruangwa. Kama mwandishi wa habari aliyeandika habari ile angeieleza vizuri, kusingekuwa na utata huu wa kusema nilikataza mikutano ya vyama vya siasa.’’

Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbowe, aliyetaka kujua serikali inasema nini kuhusu matumizi ya majeshi katika kuzuia mikutano ya vyama vya siasa.

No comments:

Post a Comment