Thursday, 3 March 2016

HALIMA MDEE, WAITARA KORTINI KWA KUJERUHI



WABUNGE wawili wa CHADEMA, Halima Mdee (Kawe) na Mwita Waitara (Ukonga), wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando, wakati wa mkutano wa uchaguzi wa Meya na Naibu Meya wa Jiji hilo.
Mbali na Halima (37) na Waitara (40), washitakiwa wengine waliofikishwa jana, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ni mfanyabiashara Rafii Juma (21) na Diwani wa Kata ya Mbezi, Ephrein Kinyafu (33).
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na polisi saa 7:23 mchana na kupandishwa kizimbani saa 7:48 mchana, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akishirikana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi na Wakili wa Serikali, Mwanaamina Kombakono, uliwasomea washitakiwa hao shitaka la kumjeruhi Theresia.
Kabla ya kuwasomea shitaka, mawakili hao wa Jamhuri waliiomba mahakama kutoa hati ya wito kwa mshitakiwa wa nne, Diwani wa Kata ya Kimanga, Manase Njema (56), ili aweze kusomewa shitaka.
Akiwasomea shitaka, Mwanaamina alidai  washitakiwa hao kwa pamoja, Februari 26, mwaka huu, katika ukumbi wa Karimjee, ulioko wilayani Ilala, Dar es Salaam, walimjeruhi Theresia na kumsababishia majeraha.
Washitakiwa hao ambao wanatetewa na Wakili Peter Kibatala akishirikiana na John Mallya, Fredrick Kiwelo, Hekima na Omary Msemo, walikana mashitaka.
Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa na kwamba hawana pingamizi juu ya dhamana.
Kwa upande wake, wakili wa utetezi Kibatala, aliiomba mahakama kuwapatia dhamana washitakiwa wanne walioko na itoe dhamana kwa masharti nafuu ikilinganishwa na kosa lenyewe.
Hakimu alitoa masharti ya dhamana kwa kila mshitakiwa kujidhamini mwenyewe na kutia saini ya dhamana ya sh. milioni mbili.
Pia, Hakimu Shaidi aliamuru kutolewa kwa hati ya wito wa kufika mahakamani kwa mshitakiwa Njema.
Washitakiwa hao waliachiwa kwa dhamana hadi Machi 16, mwaka huu, kesi itakapokuja kwa kutajwa.
Halima amesota mahabusu ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa siku mbili tangu alipokuwa akishikiliwa kwa tuhuma hizo huku Waitara akiwa ndani tangu juzi.
Viongozi mbalimbali wa CHADEMA wakiwemo wabunge na wanachama,  wamekuwa wakishinda mahakamani hapo tangu juzi, wakisubiri kuletwa mahakamani kwa viongozi wenzao.

No comments:

Post a Comment