Thursday, 3 March 2016

MAJALIWA AAGIZA KIGOGO ARDHI ASAKWE KONA ZOTE




WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha unamtafuta Ofisa  Ardhi aliyetoa hati na kibali cha kumilikisha majengo ya umma kwa Kampuni ya SK Investment ili ajieleze alikopata mamlaka hayo.
Majaliwa amesema ni lazima ofisa huyo asakwe na apatikane haraka ili aeleze alikotoa mamlaka ya kukabidhi mali ya serikali kwa kampuni hiyo, licha ya muhusika kufungua kesi mahakamani.
Hatua hiyo inakuja baada ya majengo hayo, ambayo yalijengwa kwa ajili ya ujenzi barabara wilayani hapa, ambayo yalikabidhiwa kwa serikali baada ya kumalizika kwa ujenzi huo na halmashauri kuamua kuyatumia kwa ajili ya shule ya sekondari.
Serikali iliagiza kampuni zote za ujenzi kujenga majengo ya kudumu katika maeneo yao ya kazi na wanapomaliza ujenzi, kuyakabidhi kwa serikali na kuacha kujenga majengo ya muda.
Majaliwa alisema licha ya kuwepo kwa kesi mahakamani dhidi ya suala hilo, iliyofunguliwa na Kampuni ya SK, kupinga kufutiwa kibali na hati ya kumiliki majengo hayo, lazina ofisa huyo atafutwe na atoe maelezo.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Busega, Dk. Rafael Chegeni, alimuomba Majaliwa kuingilia kati suala hilo ili majengo hayo yawe mikononi mwa serikali kama inavyotakiwa.
Chegeni alisema mara baada ya kampuni hiyo kumaliza ujenzi, majengo hayo yalichukuliwa na serikali na kuanzisha shule ya sekondari, ambapo ilishangaa kuona kampuni hiyo ikidai kuwa ni mali yake na ilipewa hati na kibali na ofisa ardhi.
Pia, aliomba serikali kuisaidia wilaya hiyo katika kuipatia ufumbuzi changamoto ya mipaka ya maeneo ya makazi na mapori ya akiba ili kuwaondolea wananchi usumbufu wa kufukuzwa katika makazi yao, yanayodaiwa kuwa ni maeneo ya hifadhi.
Majaliwa alisema suala hilo linafanyiwa kazi, ambapo mawaziri wanaohusika na masuala ya kilimo, maliasili na utalii, mifugo na tamisemi, lengo likiwa ni kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo pamoja na kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment