RAIS Dk. John Magufuli, amekuwa gumzo katika mkutano
wa viongozi wakuu wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na uchapakazi
wake, hivyo wameamua kumteua kuwa Mwenyekiti wa Jumuia hiyo.
Saa chache baada ya kupewa uenyekiti huo, Dk.
Magufuli, aliwashushia rungu watumishi wa Sekretarieti ya EAC, kuwa yeyote
atakayebainika kufuja mali za jumuia hiyo, atamtumbua jipu mara moja.
Alishangazwa na sekretarieti hiyo kutumia gharama
kubwa kuandaa mkutano huo, badala ya kubana matumzi ili fedha zitumike katika shughuli
zingine za maendeleo na kusaidia wananchi masikini wa nchi wanachama.
“Marais hawa wamefanya kosa kubwa kunichagua, sasa
kama kuna mtumishi wa jumuia anayekwenda kinyume na matakwa ya EAC,
atatumbuliwa jipu, fedha zilizotumika kuandaa mkutano huu zingeweza kununulia
madawati.
“Sekretarieti lazima mfahamu kuwa mnaongoza nchi za
watu masikini, hivyo lazima mbadilike kuendana na matarajio ya wananchi,
nitawafuatilia,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa.
Pia, kauli mbiu ya Hapa KaziTu, imeendelea
kutekelezwa kwa vitendo baada ya Dk. Magufuli, kuongoza kikao hicho kwa ustadi
wa hali ya juu.
Licha ya kuongoza kikao cha wakuu hao kwa mara ya
kwanza, Dk. Magufuli aliongoza kwa kujiamini huku wakati wote akisisitiza
wajumbe kuzingatia muda.
Awali, Tanzania ilikuwa imekwishamaliza kipindi cha
kuongoza EAC, ambapo ilitakiwa kukabidhi kijiti kwa mwanachama mwingine. Rais Jakaya Kikwete ndiye alikuwa na kijiti
hicho na kumwachia Dk. Magufuli, ambaye ndiye kilikuwa kikao chake cha kwanza.
Hata hivyo, wakuu wa EAC, Yoweri Museveni (Uganda),
Uhuru Kenyatta (Kenya), Paul Kagame (Rwanda) na Pierre Nkuruzinza wa Burundi,
walimuomba Dk. Magufuli kuendelea kuwa mwenyekiti kwa mwaka mmoja zaidi.
Hatua hiyo iliashiria wazi kuwa, viongozi hao wameridhishwa
na kumkubali Dk. Magufuli, ambaye ana miezi mitatu tu tangu aapishwe kuwa rais.
Mwenyekiti huyo mpya, amezitaka nchi wanachama
kuvumiliana na kushikamana ili kufikia maendeleo yaliyokusudiwa kwa sababu kila
nchi ina matatizo yake.
Alishauri ukanda wa Afrika Mashariki kuongozwa na
uchumi wa viwanda kutokana na kuwa na nguvukazi na ardhi ya kutosha.
Kufuatia hatua hiyo, amesema jumuia hiyo itaweza
kuuza nje bidhaa zilizosindikwa ili kuingiza pato kubwa, badala ya kuuza
malighafi ambapo hakuna faida yoyote.
“Ukanda huu
una ardhi kubwa yenye rutuba, watu wengi kiasi ambacho wanaweza kuinua uchumi
wa Afrika Mashariki kupitia viwanda,” alisema.
Alisema anaamini mkutano huo utatoka na ajenda
itakayosaidia kuanzishwa kwa suala hilo, jambo litakalosaidia kupunguza
umaskini na kupanua wigo wa ajira kwa raia wa jumuia hiyo.
Vilevile, Dk. Magufuli alishauri lugha ya kiswahili
kutumika kama lugha kuu kwa jumuia hiyo, kwa kuwa anaamini kama lugha mama,
itasaidia kuwaleta pamoja wana Afrika Mashariki, ikiwemo kuchochea maendeleo.
“Ni vema tukatumia lugha ya asili inayoeleweka na kila
mmoja, Afrika Mashariki tunacho kiswahili, tubadilike na kufanya ndio lugha ya
msingi ya mawasiliano, badala ya kiingereza, ambayo kwetu ni lugha ya kigeni,”
alisema.
Aliipongeza kwa hatua ya jumuia hiyo ya kuipokea
Sudan Kusini kama mwanachama wa EAC na uteuzi wa Liberate Mukeko wa Burundi,
kuwa katibu mkuu wake.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema jumuia
hiyo imewachagua Rais mtaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa na Museveni kuwa
wasuluhishi wa mgogoro wa Burundi.
“Lengo ni kuharakisha kutatua mgogoro huo, ambao umekuwa
dosari kwa jumuia hii, ili tuweze kusonga mbele kimaendeleo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la EAC, Kaea,
alishauri kuboreshwa kwa miundombinu ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa
katika ukanda huu na nje, kupunguza gharama za usafiri hususani wa anga na
kudhibitiwa kwa suala la rushwa, ambalo limekithiri katika sekta hiyo.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli, pia alizindua pasi
mpya za kusafiria za kieletroniki, zitakazotumika na nchi wanachama wa Jumuia
ya Afrika Mashariki.
Pasi hizo zimetengenezwa ili kuendana na viwango vya
Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO), ambazo zitamwezesha mtumiaji
kusafiri nchi yeyote duniani.
Dk. Magufuli alisema pasi hizo zitapunguza gharama za
uchapishaji zilizokuwa zikitumika katika kutayarishia pasi za karatasi.
Aidha, alisema matumizi ya pasi hizo ni salama na ni vigumu kughushiwa au kutumiwa
na mtu mwingine.
Mkutano huo uliipitisha Sudan Kusini kuwa mwanachama
mpya wa jumuia hiyo.
Akizungumzia uteuzi huo, Makamu wa Pili wa Rais wa nchi
hiyo, James Wani Igga, alisema nchi hiyo itashirikiana na
wanachama kuongeza mafanikio ya kiuchumi, kisiasa na kiusalama.
Alisema nchi hiyo kwa sasa inasonga
mbele baada ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Aliishukuru Tanzania kwa kutoa
mchango mkubwa kwenye kutafuta suluhu ya nchi hiyo, hivyo watahakikisha
wanaitumia fursa hiyo kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa hilo changa
Afrika.
ATETA NA KENYATTA, KAGAMEAwali, Dk. Magufuli, alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kando ya mkutano mkuu wa 17 wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki unaofanyika jijini hapa.
Viongozi hao wamekubaliana kuimarisha uhusiano, hususan katika masuala ya kiuchumi.
Baadhi ya maeneo waliyokubaliana kutilia mkazo katika
uhusiano huo ni kutekeleza miradi ya maendeleo inayounganisha nchi mbili,
ikiwemo miundombinu, kukuza biashara na kuzalisha ajira kupitia viwanda.
Rais Kenyatta alisema amefurahishwa kuona Rais
Magufuli yupo tayari kuhakikisha nchi ya Kenya na Tanzania zinakuwa karibu na
miradi ya maendeleo inaharakishwa.
"Kwa sababu nia yetu sisi ni kuona maendeleo
ambayo yatagusa mwananchi wa kawaida, tumalize umasikini, uchumi ukue, na hivyo
hatuwezi kufanya tukiwa tumetengana," alisema.
Kwa upande wake, Rais Magufuli alisema Tanzania na
Kenya zina kila sababu ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara, hasa katika
ujenzi wa viwanda utakaozalisha ajira kwa kuwa watu wake ni wamoja.
"Wazee wetu Mzee Kenyatta na Mzee Nyerere
walijenga mazingira mazuri ya kuwa na nchi hizi mbili wakati wakipigania uhuru,
sasa sisi vijana wao ni wakati wetu kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo,"
alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alibainisha kuwa nchi wanachama wa
Jumuia ya Afrika Mashariki zinajenga mahusiano na ushirikiano, unaolenga kupata
manufaa hayo ya kiuchumi kwa manufaa ya wananchi wake.
Aliutaja mradi mmoja wapo kuwa ni ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme kutoka Tanzania kwenda nchini Kenya kupitia Namanga na
akaongeza kuwa, Tanzania itakapoongeza uzalishaji wa umeme na kuanza kuvuna
gesi, itaiuzia pia Kenya, halikadhalika Kenya nayo itauza bidhaa zake Tanzania.
Kabla ya kukutana na Rais Kenyatta, Dk. Magufuli
alikutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambapo viongozi
hao wamekubaliana kuzidisha mahusiano kati ya Tanzania na Rwanda.
Dk. Magufuli alimhakikishia Rais Kagame kuwa serikali
itakamilisha ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, yaani ‘Standard
Gauge’ ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu.
Rais Kagame alimpongeza Dk. Magufuli kwa uongozi wake
bora uliolenga kuimarisha uchumi, ikiwemo kuimarisha Bandari ya Dar es Salaam,
ambayo Rwanda inaitegemea na ujenzi wa reli ya kati, ambayo pia ni tegemeo
kubwa kwa uchumi wa Rwanda.
No comments:
Post a Comment