Thursday, 3 March 2016

DAR YATENGA BILIONI 343.5/- UTENGENEZAJI BARABARA


MAMLAKA zinazosimamia matengenezo ya barabara mkoani Dar es Salaam, zimetenga jumla ya  sh. bil. 343.5 kwa ajili ya  mipango ya matengenezo ya barabara  kwa kipindi cha mwaka wa fedha  2016/17.

Kiasi hicho cha fedha ni  sawa na asilimia 346.8, ambapo ni ongezeko la  sh.  bil. 266.6, ikilinganishwa na fedha zilizotengwa  katika kipindi cha mwaka wa fedha unaoendelea, 2015/16, ambapo zilitengwa  sh. bilion 76.8 kwa ajili ya shughuli hiyo.

Akifungua kikao cha kwanza cha bodi ya barabara mkoani humo, Mkuu wa Mkoa huo, Said  Sadiki, alisema,  fedha hizo zinatoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato.

Alisema kwa upande wa Halmshauri ya  jiji la Dar es Salaam, fedha zilizotengwa kutoka katika vyanzo vyake vya mapato ya ndani ni sh.bilioni  1.3 na kutoka  serikali kuu (LGCDG) ni sh bilioni moja,  ambapo jumla ya fedha zote ni  sh. bil. 2.3.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, fedha zilizotengwa   ni kutoka  Mfuko wa Barabara (Road Fund), sh. bilioni 7.1, vyanzo vya ndani sh.bilioni 3.6,  serikali kuu sh. bilioni 7.8 na Benki ya Dunia sh. bilioni 48.3, ambapo jumla ni sh. bilioni 66.9.

“Kwa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, fedha zilizotengwa kutoka Mfuko wa Barabara ni sh. bilioni 6.00, vyanzo vya ndani sh. bilioni 3.8, serikali kuu sh. bilioni 1.8 na Benki ya Dunia sh. bilioni 57.6,  ambapo jumla ni  sh.68.7,”alisema Sadiki.

Alisema Wakala wa Barabara mkoani humo (TANROADS), fedha zilizotengwa ni sh. bilioni 127.1, ambapo matengenezo ya kawaida sh.bilioni 42 .2  na miradi ya maendeleo sh.bilioni 84.9.

Kwa upande wa Halmshauri ya Wilaya ya Kinondoni,  fedha zilizotengwa ni sh.bilioni 78.4, ambapo kutoka mfuko wa barabara ni sh. bilioni 12.8, vyanzo vya ndani sh.bilioni 1.5, serikali kuu sh. milioni  454 na  Benki Kuu sh. bilioni 63.6.

Hata hivyo, Sadiki aliitaka halmashauri hiyo  kuongeza fedha kutoka katika  vyanzo vyake vya mapato ya ndani kutokana na halmashauri hiyo kuwa na mtandao mkubwa wa barabara kuliko halmashauri zingine za mkoa huo.

“Ni matumaini yangu  kuwa kiasi hiki cha fedha kitatumika kama ilivyokusudiwa ili kupata thamani halisi ya fedha  hizo.Matumizi  thabiti ya fedha hizo yatasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na baadhi ya changamoto  zilizopo za miundo mbinu  ya barabara za mkoa wetu. Kusema ukweli hali ya barabara nyingi siyo nzuri,”alisema Sadiki.

Aliongeza: ” Ninachukua fursa hii kuzitaka mamlaka husika  kuanza kutekeleza mipango kazi yake  kwa kuzingatia  taratibu  husika  mara baada  ya mwaka wa fedha kuanza.”

Alisema mwaka ujao, mkoa wa Dar es Salaam kupitia Ofisi ya Rais  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), utaanza uboreshaji  wa miundombini mbalimbali, ikiwemo barabara  chini ya mradi ujulikanao  kama Dar es Salaam Metropolitan Developmet (DMDP).

Kikao hicho kilichowahusisha wabunge na wajumbe kutoka mamlaka mbalimbali za mkoa wa Dar es Salaam, kilipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya vikao vilivyopita,  kupokea taarifa  ya ziara ya wajumbe wa bodi iliyofanywa katika wilaya zote za mkoa, walipotembelea miradi mbalimbali ya matengenezo ya barabara.

Pia, kilipokea  na kujadili taarifa za matengenezo ya barabara hadi kufikia robo ya pili  ya mwaka wa fedha 2015/16, kutoka TANROAD mkoa wa Dar es Salaam,  Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka  (DART) na mamlaka za serikali za mitaa za halmashauri zote tatu mkoani humo.
 

No comments:

Post a Comment