Thursday, 3 March 2016
DOVUTWA AMCHANACHANA MBOWE
VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vinadaiwa kupoteza muelekeo wa misimamo yao na kutia aibu dhana nzima ya upinzani.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jana, Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema hilo limejidhihirisha baada ya Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Freeman Mbowe, kupinga msimamo wa Rais Dk. John Magufuli wa kufuta safari za nje na kutumbua majipu.
Alisema UKAWA wamekuwa kituko sasa kwa kauli zao wanazotoa, ambazo hazina msimamo tena na badala yake wanaonekana wanasiasa wababaishaji.
"Nawakosoa UKAWA kwa sababu wao wanajinasibu ni wapinzani, lakini kwa mwenendo wao wanatia aibu upinzani wote, hivyo ni vyema wananchi wajue nani mwanasiasa na kiongozi na ni nani mwanasiasa mbabaishaji na mpiga dili.
"Pili, nawaonea huruma UKAWA kwa sababu siasa za kulipua mabomu kupitia nyaraka za serikali sasa hazipo, Dk. Magufuli aliyeko madarakani anafyatua mwenyewe hayo mabomu," aliongeza.
Dovutwa alisema UKAWA walijijengea muonekano wa kupinga misafara ya nje ili fedha zinazopatikana zitumike katika maeneo ya huduma za jamii, ambapo ilifikia hatua safari za nje kwa serikali kuwa miongoni mwa ajenda zao kwenye kampeni za uchaguzi.
"Alipoingia Ikulu, Rais Magufuli akasitisha safari za nje, sasa kinyume cha msimamo wao wa kupinga safari hizo, hivi sasa UKAWA wanapinga Rais kufuta hizo safari na kwenda mbali kwamba bila kujitambulisha nchi za nje, maendeleo hayatapatikana na itakuwa vigumu kujulikana na kusaidiwa.
"Sasa UKAWA jema lipi? Rais Magufuli asafiri au asisafiri? Kwa maana hiyo nawaona UKAWA wamekosa kielelezo cha imani yao ya upinzani," alisema.
Alisisitiza kwamba kinachoshangaza zaidi ni Mbowe kutilia shaka utumbuaji wa majipu unaofanywa na Rais Magufuli na serikali yake na kwamba, ni kituko kwa sababu umoja huo walikuwa wanalalamika juu ya utendaji dhaifu wa serikali usiokuwa na uwajibikaji.
Alisema Rais Magufuli ameyasikia malalamiko ya UKAWA, anasimamia watendaji, hivyo watendaji dhaifu anawashusha na kuwapandisha wengine wapya, kitendo ambacho kinawapa hofu ya kupoteza wafadhili wao, hivyo wanaiona hatari iliyoko mbele yao.
Dovutwa aliongeza kuwa hata kwenye safari za Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, ambazo zilikuwa na manufaa, pamoja na kupinga, lakini kuna wabunge wa UKAWA walikuwa wakifaidika nazo.
Aliwataka viongozi wa umoja huo kunyamaza na kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli kwa maendeleo ya taifa, kwa sababu upinzani si kupinga kila kitu.
00000
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment