Tuesday 19 April 2016

RAIS MAGUFULI AMTUMBUA JIPU MKURUGENZI WA JIJI LA DAR ES SALAAM, WILSON KABWE



RAIS Dk. John Magufuli amemtumbua jipu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe kutokana na tuhuma mbalimbali za ubadhirifu.

Uamuzi wa Rais Magufuli kumtumbua jipu Kabwe, ulikuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumlalamikia kwa kuisababishia serikali hasara ya sh. milioni 500.

Mara baada ya Makonda kutoa malalamiko hayo kwa Rais Magufuli, mkuu huyo wa nchi aliwauliza wananchi iwapo amtumbue jipu Kabwe papo hapo.

Kwa pamoja, wananchi hao walinyoosha mikono hewani kuashiria kuukubali uamuzi huo na ndipo Rais Magufuli alipotangaza kumsimamisha kazi Kabwe.

Aidha, Rais Magufuli alimpongeza Makonda kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi tangu alipoteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni na baadaye kupandishwa kuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam.

Mapema wiki hii, Makonda alisema hayuko tayari kuendelea kufanyakazi na Kabwe, kutokana na kuisababishia serikali hasara ya sh. milioni 500, katika kipindi cha mwaka mmoja, kutokana na kuingia mikataba mibovu.

Aliitaja mikataba hiyo kuwa ni pamoja na ya zabuni mbalimbali, kinyume cha sheria, zikiwemo kampuni  inayokusanya ushuru katika Stendi Kuu ya Mabasi Ubungo na kampuni ya kukusanya ushuru wa maegesho jijini Dar es Salaam (NPS).

No comments:

Post a Comment