Thursday, 3 March 2016

VIGOGO WASALITI CCM KUSAKWA KILA KONA


 
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa, ameziagiza kamati za maadili na kamati za siasa za wilaya kukaa chini na kuwatambua watu wote waliokisaliti Chama, wakati wa uchaguzi ili waweze kushughulikiwa bila kuonewa  haya.

Amewahimiza viongozi wa Chama mkoani hapa, kuisimamia serikali ili iweze kutekeleza na kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Kimbisa alitoa kauli hiyo jana, katika kikao cha halmashauri kuu ya mkoa, kilichokuwa na ajenda ya kufanya tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Alisema katika kikao cha Kamati ya Siasa cha Mkoa, wamekubaliana kuwa kamati za maadili zitumie ushahidi kuwajua wasaliti bila ya kuonea mtu na majina yao yapelekwe kwao.

"Sisi hatuna tatizo muwafute, muwajue, muwe na ushahidi na muwajadili mtuletee, msionee mtu, mtende haki kwa sababu kuna Mungu, msifanye hivyo kwa sababu ya kumzuia mtu asigombee tena kipindi kingine, hapo mnatenda dhambi," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa vikao hivyo vijadili kwa viwango kwa kutumia ushahidi ili kweli mtu aonekane ameshiriki na kwa watu hao, adhabu zipo, ikiwemo karipio, onyo na adhabu nyingine na kwa wengine kuondolewa kabisa baada ya kuona hafai.

Alitolea mfano katika wilaya ya Chemba, ambapo kulikuwa na mgombea mmoja wa udiwani Sambala na kumpa jina la karata tatu, aliyekuwa anaamka asubuhi na kusema kura ya udiwani apewe yeye, lakini ya urais apewe mgombea wa Chadema.

"Sina msamaha na mtu, mnanijua sihongi, sihongeki. Kama kuna mtu ametusaliti kama Sambala na ushahidi upo, msionee, mtuletee, watu hao ni wa kwanza wanaotakiwa kutumbuliwa, mtu aseme mimi nahama naenda chama kingine, huyo hatuna matatizo.

"Mke kakuacha kaenda kwa bwana mwingine wewe una wasiwasi naye, tatizo ni kuwa mke yupo ndani halafu anakusaliti, habari zote za ndani mlizoziongea, jirani wote wanazo, huyo anafaa talaka tatu, haiwezekani tukavumilia kiasi hicho,” alisema.

Kimbisa aliwataka kwenda kuisimamia serikali ili itekeleze majukumu yake ya kuwapelekea wananchi maendeleo kama ilivyoahidi ili 2020, kazi iwe laini na Chama kisipate shida kutafuta kura.

"Nendeni mkasimamie serikali maana hata tukivaa mashati ya kijani kiasi gani, kama serikali hatuwezi kuisimamia katika hatua zetu, shati la kijani halina maana wala njano, kama maji hayapo katika maeneo yetu, ukivaa  shati la kijani halina maana," alisema Kimbisa.

Aidha, aliwapongeza wajumbe wa kikao hicho kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuhakikisha Chama kinashinda kwa kishindo.

"Siri ya ushindi ni 'team work', mshikamano umoja na utulivu, tuendelee hivyo hivyo, fitina hazikosekani, msifuate wanaopiga  fitina wamefilisika sera, achana nao tujenge mkoa wetu kwa wakati ujao, tumemaliza uchaguzi huu ndio mwanzo  wa uchaguzi wa 2020," aliongeza Kimbisa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, amewataka kujipanga kila mtu kwa nafasi yake ili kuhakikisha changamoto mbalimbali zilizopo katika mkoa huo zinatatuliwa, ikiwemo madawati, maabara na kutokomeza mlipuko wa kipindupindu katika maeneo yao.

Awali, Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Jamila Yusuph, akimkaribisha mwenyekiti alisema akidi ya wajumbe imekidhi, ambapo wajumbe waliohudhuria ni 70 kati ya 87.

No comments:

Post a Comment