Thursday, 3 March 2016

MAJALIWA AONYA LUGHA CHAFU KWA WAUGUZI





Na Khadija Mussa, Busega
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka madaktari kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa na  kumuagiza Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu, kusimamia suala hilo na kurekebisha maeneo atakayokuta yana matatizo.
Amesema watumishi wa umma wanatakiwa kuhakikisha wanawapokea, wanawasikiliza na kuwahudumia vizuri wananchi wanaokwenda kufuata huduma bila ya kujali itikadi zao.
Majaliwa  amesema serikali imeweka mikakati itakayowezesha watumishi wote kulipwa maslahi na haki zao kwa wakati, hivyo aliwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana, alipokuwa akizindua ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya ya Busega, katika siku  ya kwanza ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani Simiyu.
Alisema watumishi wanatakiwa kuhakikisha wanapokea, wanawasikiliza na kuwatatulia matatizo yao wananchi wote wanaokwenda katika maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kutatuliwa matatizo yao.
Pia, amewataka watumishi hao kuondoa hofu kwa sababu jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanawahudumia wananchi bila ya kujali uwezo wao, makabila yao wala itikadi za vyama.
Alisema watumishi lazima wajiridhishe kwa utendaji na wanatakiwa kuwa waaminifu ili wafanye kazi kwa bidii na serikali imejipanga katika kuhakikisha inaboresha mazingira yao.
Aidha, aliwataka madiwani kukubaliana na utaalamu unaotolewa na wataalamu na wapunguze kubishana sana katika halmashauri, badala yake wasimamie na kufuatilia utekelezaji wa mambo wanayokubaliana.
Alisema fedha zinazopelekwa lazima zitumike kama ilivyokusudiwa na madiwani lazima wakague. Pia alisema viongozi wa CCM nao wapitie na kuangalia utekelezaji wa Ilani.
Pia, aliwataka watumishi wa wilaya ya Busega kuwa wavumilivu na kufanya kazi kwa bidii wakati serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa wilaya hiyo mpya.
Awali, Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Eraston Mbwilo aliiomba serikali kuusaidia mkoa huo, ambao unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa majengo kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya.
Mbwilo alisema hadi sasa hawana majengo ya ofisi na makazi kwa ajili ya mkuu wa mkoa na baadhi ya wilaya, jambo linalosababisa kufanya kazi katika mazingira magumu.
Majaliwa alisema tayari suala hilo linafanyiwa kazi kwa kuyaagiza mashirika ya fedha, likiwemo NSSF, kwenda kujenga majengo katika mikoa na wilaya mpya, badala ya kuendelea kujenga katika maeneo ambayo tayari yameshaendelea.
Hata hivyo, aliwataka watumishi wote wa halmashauri hiyo, ambao wanaishi nje ya wilaya hiyo, wahamie makao makuu ya wilaya hiyo na kupanga nyumba katika maeneo ya karibu wakati serikali ikiendelea na mchakato wa ujenzi.

No comments:

Post a Comment