Wednesday, 2 March 2016

KESI YA KUPINGA UBUNGE KILOMBERO KESHOKUTWA




MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Ijumaa ijayo itasikiliza pingamizi la awali lililowasilishwa katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa Jimbo la Kilombero, mkoani Morogoro, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho wa CCM, Abubakar Asenga.

Asenga, kwa kupitia mawakili wake, Sam Mapande na Onesmo Mpenzile, alifungua kesi hiyo dhidi ya mbunge wa jimbo hilo, Peter Lijualikali, msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria mkuu wa serikali.

Jaji Edson Mkasimongwa, alipanga juzi tarehe hiyo ya kusikiliza pingamizi hilo la awali.

Baada ya kufungua kesi hiyo namba 5,2015, aliiomba mahakama kutangaza kwamba ushindi wa Lijualikali ni batili kwa sababu uchaguzi haukuzingatia sheria.
Lijualikali akiwakilishwa na Wakili Tundu Lissu, aliwasilisha utetezi wake na pingamizi la awali akiipinga kesi hiyo.

Katika pingamizi hilo, Lijualikaji anapinga shauri hilo akidai halina maelekezo ya kutosha kufanya wao kujitetea na halijafunguliwa kwa kufuata kifungu cha sheria husika.

Juzi, shauri hilo lilikuja mbele ya Jaji Mkasimongwa kwa ajili ya uamuzi kutokana na kubaini kwamba, mjibu maombi wa kwanza (mbunge), aliwasilisha utetezi wake na pingamizi la awali kabla ya wakati.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Mkasimongwa alipokea utetezi huo na pingamizi hilo la awali, baada ya kuzingatia mazingira ya shauri hilo kwamba, mjibu maombi ana haki ya kujitetea, hivyo hata kama akiyatupilia mbali, haimuondolei (mjibu maombi huyo), sifa ya kuleta utetezi huo.

Jaji Mkasimongwa alisema mjibu maombi huyo aliwasilisha utetezi huo baada ya kupokea taarifa ya wito mahakamani, jambo ambalo lilikuwa likimsumbua iwapo majibu hayo yaliletwa kwa wakati sawa au la.

Alisema kutokana na hilo, mahakama iliwaomba mawakili wa pande zote husika kuwasilisha hoja zao iwapo wanaona majibu hayo yameletwa kwa wakati sawa au la.

Jaji Mkasimongwa alisema taarifa za kuitwa mahakamani zinatolewa kwa lengo la kupeleka ujumbe zinazoubeba kwa mtu anayetajwa, ambapo hiyo aliyopewa mjibu maombi wa kwanza, ilikuwa inaeleza kesi imefunguliwa dhidi yake na nakala imeambatanishwa na itakuwepo siku atatakiwa afike mahakamani na kuleta utetezi wake.

Alisema anatofautiana na hoja za Wakili Lissu kwamba maneno yaliyoko katika notisi hayaungi mkono na kile kilichoelezwa na wakili huyo. Alisema mahakama wakati wowote haikumuamuru mjibu maombi huyo awasilishe utetezi wake na wala notisi hiyo haikumtaka afanye hiyo.

Kuhusu kuyafuta majibu hayo au la, Jaji Mkasimongwa alisema amezingatia mazingira ya shauri hilo na jibu hapana, kwa kuwa mjibu maombi ana haki ya kujitetea na kwamba hata akiyaondoa, hakutaharibu sifa ya kufanya hivyo.

Wakati wa usikilizwaji wa hoja hiyo, Wakili Lissu alidai mbunge huyo amewasilisha majibu hayo sawa mahakamani na iwapo itaona hayajaletwa kwa wakati, kasoro hiyo haiwezi kuyafanya yafutwe. Lissu aliiomba mahakama isiyatupilie mbali maombi hayo kwa kasoro kama hiyo.

Kwa upande wake, Wakili Mpenzile anayemwakilisha Asenga, alidai kanuni za uchaguzi hazielezi ni lini na wakati gani mtu anapaswa alete majibu yake.

Wakili huyo alidai kuwasilisha majibu mahakamani kabla ya wakati ni sawa na kuyawasilisha baada ya wakati, hivyo aliomba  yafutiliwe mbali.

No comments:

Post a Comment