MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan,
amewataka wana-CCM mkoani Tanga, kuhakikisha wanajisafisha na kuongeza uadilifu,
ikiwa ni pamoja na kuzuia mianya ya ukwepaji wa mapato unaofanyika kupitia
bandari bubu zilizopo Pangani na Mkinga.
Alitoa wito huo juzi, kwenye
mkutano wake na makatibu wa CCM, makatibu uenezi, makatibu uchumi, wenyeviti wa
halmashauri na viongozi wengine, ambapo alielezea kushangazwa kwake na bandari
hizo bubu kutumiwa na baadhi ya watu ili kukwepa kodi za serikali.
Katika mkutano wake huo, Samia alisema
litakuwa jambo la busara kama wakazi wa Tanga, wataanza kulishungulikia wenyewe
suala hilo kabla ya serikali kuu kuwanyooshea vidole, akisema kwamba kufanya
hivyo itakuwa sehemu ya mchango wao kuunga mkono jitihada za serikali.
Alisema serikali iliyoko
madarakani imeanza kuchukua hatua kwa kubana vitendo vya ufisadi na ubadhilifu
wa fedha, ambapo wana-CCM ambao ndio wasimamizi wa Ilani ya Chama chenye
serikali iliyoko madarakani, wanatakiwa kuongoza mapambano dhidi ya vita hiyo inayoendelea.
“Serikali imeanza vizuri katika
kuchukua hatua kwa vile inachukia vitendo vya ufisadi na ubadhilifu wa namna mbalimbali,
kwa hiyo mnatakiwa kuiunga mkono. Hapa Tanga kuna bandari bubu za Mkinga na
Pangani, zinazotumika kukwepa mapato, ni vyema mkaliona hili kabla
hamjanyooshewa vidole,” alisema.
Mbali na hilo, Makamu wa Rais
pia alitumia fursa hiyo kuwataka wana-CCM kuimarisha umoja miongoni mwao huku
wakiimarisha jumuia zao, lengo likiwa kukiwezesha Chama kuendelea kushika dola
na nchi kuwa katika hali ya amani na utulivu muda wote.
Aliongeza kuwa kuna kila sababu
kwa jumuia hiyo kufanya kila jitihada katika kuhakikisha zinaendesha shughuli
zao kwa tija, akitolea mfano uendelezaji wa miradi, lengo likiwa kukiwezesha Chama
kuwa na nguvu za ziada huku akisisitiza kuwa miradi isiyo na tija ni sawa na
hakuna.
No comments:
Post a Comment