Wednesday, 2 March 2016

SERIKALI YAIZUIA TANESCO KUNUNUA TRANSFOMA NJE




WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amelipiga marufuku Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuanzia sasa kuacha kununua transfoma za kufua umeme nje ya nchi, badala yake zinunuliwe za viwanda vya ndani.
Amesema hakuna sababu ya shirika hilo kuendelea kuagiza trasfoma nje ya nchi wakati kuna viwanda vya ndani, ambavyo serikali ina ubia na zinatengeneza vifaa hivyo vya kisasa na vyenye ubora.
Serikali inamiliki asilimia 20 ya hisa katika kiwanda cha TANELEC, ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa vifaa vya umeme, ikiwemo transfoma kilichoko jijini Arusha.
Akizungumza jana, wakati wa ziara yake kiwandani hapo, Profesa Muhongo, alieleza kushangazwa na kusikitishwa na hatua ya TANESCO kuacha kununua vifaa kutoka kwenye kiwanda hicho na kukimbilia nje kwa kigezo cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
“Kwa kuanzia ni marufuku kuagiza transfoma za nje na mchukue za kwenu, ambako mnamiliki hisa asilimia 20 na ukiweka hisa za Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) wanaomiliki asilimia 10, zinakuwa hisa asilimia 30, halafu mnakimbilia nje,” alisema.
Alisema sheria ya manunuzi ililetwa na wapiga dili na wanaonufaika ni kikundi cha watu wachache na wanafahamu sababu za kuipenda sheria hiyo ambayo inazuia Watanzania kununua bidhaa zao na kuwataka wanunue za nje ya nchi.
Alisema suala la ununuzi wa transfoma hizo nje ya nchi umegubikwa na rushwa, sababu hata tenda iliyoshinda kuuziwa TANESCO transfoma ni ya Quality Group,  ambayo ni ya mzawa na Inter Trade ya nje ya nchi, ambao wote si wazalishaji wa transfoma, badala yake wanaagiza kutoka India.
Alisema katika mazingira hayo, kunaashiria kuwepo kwa vitendo vya rushwa kwani, TANELEC, ambayo ni ya kitanzania na TANESCO na NDC zina hisa, zimekosa zabuni hiyo.
“Yaani hii ni sawa na mtu asage unga wa kutumia nyumbani kwake na anatokea
mtu anakataza kutumia unga huo, badala yake unatakiwa kununua toka
nje ya nchi. Huo ni uhuni na mahitaji yenu Tanesco ni trasfoma 1,500
hadi 2,000 kwa mwaka, hivyo uwezo huo upo wa kuzipata hapa hapa nchini na
mnasema ni bora, hivyo hakuna sababu ya kutangatanga,” alisema.

Aidha, alimwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Nishati na Madini kuweka bayana kuwa Sheria ya Manunuzi ya Umma ni kandamizi na imekuwa ikiliingiza taifa hasara ya mabilioni ya shilingi kwa manufaa ya wachache, hivyo ni vyema ikabadilishwa.
Pia, aliwataka wakandarasi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), kutumia
vizuri fedha za walipakodi zaidi ya sh. bilioni 877, zilizotolewa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini ili kufanikisha walengwa na kukidhi matakwa ya serikali ya kusambaza umeme kila kijiji nchini.

Meneja wa Kiwanda cha TANELEC,  Zahir Saleh, alimwomba waziri huyo kusaidia kiwanda hicho kufanikisha lengo la kuzalisha transfoma 10,000, ambapo sasa wanazalisha 7,000, kutokana na TANESCO kutonunua bidhaa hizo tangu sheria ya
manunuzi ilipoanza.

“Kutokana na hili tunaomba serikali ingeweka sheria angalau kuwabana Watanzania kununua bidhaa zao kwa asilimia 40, kama ilivyo kwa nchi ya Kenya, ili kuweza kuleta ari ya kuweka viwanda zaidi nchini. Pia iambatane na kuondoa sheria za kuwabana raia kununua bidhaa zao,” alisema.
Zahir alisema kutokana na sheria hiyo kuwanyima TANESCO kununua transfoma zake, imesababisha kiwanda kupunguza wafanyakazi 60 kwa sababu uzalishaji umepungua.
Kaimu Meneja Mwandamizi wa Manunuzi nchini, Jasson Katule, alisema tenda za kampuni zilizoshinda kutokana na sheria ya manunuzi ni Inter Trade, ambayo ilishinda kwa Dola za Marekani milioni tano na Quality Group, ilishinda kwa Dola za Marekani milioni tatu.
Hata hivyo, alisema kutokana na maagizo na maelekezo ya Profesa Muhongo, kila kitu kinawezekana kwa kuwa hali hiyo imejitokeza kutokana na kulazimika kufuata sheria hiyo.

No comments:

Post a Comment