Wednesday, 2 March 2016

SERIKALI YACHARUKA BALOZI SEFUE KUCHAFULIWA




SERIKALI imekanusha vikali taarifa zilizotolewa na gazeti moja la kila wiki, zikimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuwa ni jipu lenye kutakiwa kutumbuliwa kutokana na kuhusishwa na tuhuma mbalimbali.
Pia, imelitaka gazeti hilo, kukanusha uongo na uzushi wa taarifa ilizozichapisha kwa kuiomba radhi pamoja na watu wote walioumizwa na uzushi huo, akiwemo Balozi Sefue.
Imeonya kuwa endapo litashindwa kufanya hivyo, litafikishwa mara moja kwenye Sekretarieti ya Maadili pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU.
Katika gazeti hilo, toleo namba 404, lililochapishwa Februari 29, mwaka huu, lilimtuhumu Balozi Sefue kushawishi kufanyika kwa uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha, Katibu Mkuu huyo kiongozi, alituhumiwa kuhusika katika utoaji tenda kwa Kampuni za CRJE na UGG kupewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na Reli ya Dar es Salaam hadi Kigali.
UTEUZI MSD
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na serikali, Katibu Mkuu huyo hakuhusika kwa namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa, uteuzi huo ulitekelezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa, ikiwemo nafasi hiyo kutangazwa na bodi Novemba 20, mwaka 2013.
Katika usaili wa kuziba nafasi hiyo, ambao uliendeshwa na kampuni huru iliyopewa majukumu na MSD, mapendekezo ya majina matatu yalipelekwa kwa Rais mstaafu, Jakaya Kikwete pamoja na kwa aliyekuwa Waziri wa Afya, Dk. Seif Rashid.
Baada ya kumalizika kwa mchakato huo, Mkurugenzi aliyeteuliwa kushika wadhifa huo, hakuwa na mahusiano yeyote wala kufahamiana na Balozi Sefue.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, alichofanya Balozi Sefue ni kutangaza uteuzi wa mkurugenzi huyo baada ya Rais kumteua.
Aidha, gazeti hilo lilidai, tangu kuanzishwa kwa MSD, haijawahi kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu asiye Mfamasia, taarifa ambazo siyo za kweli.
TUHUMA DHIDI YA CRJE
Kwa mujibu wa gazeti hilo, lilimtuhumu Balozi Sefue, kumuhusisha na kampuni hiyo ya ujenzi hadi kupewa tenda ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.
Kipindi ambacho CRJE, inapewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Oktoba 2007, Balozi Sefue hakuwa Katibu Mkuu Kiongozi na hakuhusika na mchakato wa kuipatia tenda kampuni hiyo.
Pia, wakati wa kumpata mkandarasi wa Daraja la Kigamboni, ulipoanza Machi, 2011, Balozi Sefue, alikuwa Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, (UN).
Aidha, wakati mkataba wa ujenzi wa daraja hilo ulipotiwa saini Januari 9, mwaka 2012, Balozi Sefue alikuwa na wiki moja tangu kushika wadhifa wa Katibu Mkuu Kiongozi.
Licha ya gazeti hilo kuandika kuwa CRJE ndiyo iliyopewa tenda ya ujenzi, lakini ukweli ni kwamba kampuni iliyoshinda tenda hiyo ni China Major Bridges Engineering Company (BCEC) kwa kushirikiana na Kampuni ya China Railway Construction (CRCEG).
KUIPIGIA CHAPUO UGG NA MASWI
Katika ufafanuzi huo, ulieleza kuwa hakuna kampuni yenye jina la UGG iliyowahi kuonyesha nia ya kujenga reli ya kati, hivyo kuthibitisha kuwa habari hiyo ni ya upotoshaji.
“Hivyo Balozi Sefue, hakuhusika katika kuchagua kampuni ya kupewa tenda hiyo kwa sababu yeye sio sehemu ya wenye mamlaka ya kutoa tenda,”imeeleza taarifa hiyo ya serikali.
Gazeti hilo la pia liliandika taarifa kumuhusisha Katibu Mkuu huyo Kiongozi kumsafisha aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, taarifa ambazo imeelezwa kuwa hazina ukweli.
Kufuatia tuhuma hizo, serikali imewataka waandishi wa habari kuzingatia taaluma na weledi, ikiwemo kuacha kutumiwa na watu kuendeleza ajenda binafsi zisizokuwa na maslahi kwa taifa.

No comments:

Post a Comment